1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi wa reli, viwanja vya ndege wagoma tena Ujerumani

7 Machi 2024

Mamia kwa maelfu ya wasafiri wamekwama nchini Ujerumani kufuatia mgomo mpya wa wafanyakazi wa reli na viwanja vya ndege wanaodai nyongeza ya mishahara. Taifa hilo limekumbwa na migomo ya mara kwa mara ya wafanyakazi.

https://p.dw.com/p/4dHIT
Treni za kampuni ya Deutsche Bahn
Safari za treni za mwendokasi zimeathirika kufuatia mgomo huo wa siku mbili UjerumaniPicha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

Taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya limekumbwa na migomo ya mara kwa mara kwa miezi kadhaa wakati ambapo wafanyakazi na waajiri katika sekta mbalimbali wakivutana kuhusu masharti ya kazi katikati mwa mfumuko mkubwa wa bei na kudorora kwa shughuli za biashara.

Migomo ya wafanyakazi imezikumba sekta za usafiri, maduka makubwa ya kujihudumia, au Supermarkets na utumishi wa umma miongoni mwa maeneo mengine ya maisha ya umma. Kwa mara ya tato tangu Novemba 2023, wafanyakazi wa reli wamesusia kazi, wakianza mgomo wa saa 35 katika huduma za usafirishaji mizigo hapo jana, na usafirishaji wa abiria kuanzia leo asubuhi.

Ndege za Lufthansa katika uwanja wa Munich
Safari za ndege pia zimeathirika kufuatia mgomo wa shirika la ndege la LufthansaPicha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Urefu wa mgomo huo unakusudiwa kutilia mkazo matakwa muhimu ya chama cha madereva wa treni cha GDL kupunguza muda wa juma la kazi kwa masaa 35 kutoka 38 ya sasa. Reinhard Logocki, ambaye alifanikiwa kuwasili kituo kikuu cha jiji la Berlin akitokea Bonde la Ruhr, alisema Wajerumani wa kawaida wamejikuta mara kwa mara njiapanda katika mzozo huu unazodi kuwa mbaya.

Nadhani baada ya muda mrefu, washirika wa mazungumzo hawapaswi tena kutekeleza hili juu ya migongo ya abiria. Hayo ni maoni yangu.

Soma pia: Abiria nchini Ujerumani watatizika na migomo ya treni na viwanja vya ndege

Wafanyakazi wa reli wamekuwa wakifanya migomo ya kujirudia kudai nyongeza ya mishahara kuwasaidia wanachama wao kumudu gharama kubwa za maisha zinazosababishwa na mfumuko wa bei. Mgomo wa madereva wa treni mnamo Januari ulisababisha usumbufu kwa maefu ya wasafiri kwa siku kadhaa.

Deutschland, Köln | Mehrtägiger Streik der Lokführergewerkschaft GDL
Vituo vya treni vilisalia bila watu baada ya chama cha wafanyakazi kutangaza mgomo wa siku mbiliPicha: Marc John/IMAGO

Shirika la Reli la Ujerumani, Deutsche Bahn, limelaani mgomo huo, likisema limetoa muafaka wa hadi nyongeza ya asilimia 13 ya mshahara. Msemaji wa shirika hilo Achim Stauss, aliliambia shirika la utangazaji wa umma la ZDF, kwamba ni karibu asilimia 20 tu ya treni zake za masafa marefu ndiyo zinafanya kazi, huku kukiwa na tofauti kubwa kati kati ya majimbo.

Mkuu wa chama cha GDL Claus Weselsky alisema mapema wiki hii kwamba migomo mingine itatangazwa kila watakapoona ni wakati sahihi, na hawatatoa tena taarifa ya masaa 48 kabla kama ilivyokuwa siku za nyuma. Msimo huo mkali wa Weselsky umekosolewa na waziri wa usafiri Volker Wissing, ambaye amesema anapoteza subira na migomo hiyo.

Wissing ameliambia shirika jengine la utangazaji wa umma la Ujerumani, ARD, kwamba wale wanaotekeleza haki yao ya kugoma wanapaswa pia kubeba wajibu, na kwamba hilo linamaanisha kujadiliana kwa njia yenye kujenga.

Wakati huo huo, wafanyakazi wa mizigo wa shirika la ndege la Luftansawamefanya mgomo kuanzia leo alfajiri hadi Jumamosi jioni, huku shirika hilo likisema limeweza tu kudumisha asilimia 10 hadi 20 ya ratiba yake ya safari zake. Viwanja vinavyotazamiwa kuathirika zaidi na mgomo huu ni pamoja na Frankfurt, ambao ndiyo kituo kikuu cha usafiri wa ndege nchini Ujerumani.

dpa