Wafadhili waahidi kuipa Palestina dola milioni 242 | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wafadhili waahidi kuipa Palestina dola milioni 242

Polisi ya Palestina kuimarishwa

Wafadhili wa kimataifa waliokutana leo mjini Berlin wameahidi kutoa dola milioni 242 za kimarekani kwa ujenzi wa miundo mbinu ya usalama katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Ujerumani.

Fedha hizo zitakabidhiwa mamlaka ya ndani ya Wapalestina katika kipindi cha miaka mitatu ijayo na zitatumika katika hatua za mashinani kama vile usajili wa maafisa zaidi wa polisi, ujenzi wa vituo vya polisi na mahakama ili kuboresha mazingira ya kuundwa kwa taifa huru la Wapalestina.

Fedha hizo zitatolewa kutoka kwa kiwango cha fedha zilizoahidiwa kwenye mkutano wa jumuiya ya kimataifa uliofanyika mnamo mwezi Disemba mwaka jana mjini Paris Ufaransa.

Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 40 na mashirika ya kimataifa wamehudhuria mkutano wa mjini Berlin akiwemo waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Condoleeza Rice, waziri mkuu wa mamlaka ya Palestina, Salam Fayad na waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel, Tzipi Livni.

Mkutano wa mjini Berlin umetuwama katika juhudi za kuisaidia mamlaka ya Palestina kuiopa mafunzo ya kisasa polisi yake na kujenga mfumo mpya wa sheria katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan.

Akizungumza kwenye mkutano huo waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier amesema, ´Nadhani tunahitaji polisi ya Palestina yenye ujuzi mzuri na iwezeyo kufanya kazi yake. Polisi iliyopata mafunzo mazuri kwa kushirikiana na mahakimu, waongozaji mashtaka wa serikali na vyombo vya sheria vinavyofanya kazi, inaweza kuwapa Wapalestina usalama muhimu wanaohitaji.´

Ujerumani inaunga mkono suluhisho la mataifa mawili katika kuutanzua mzozo baina ya Waisraeli na Wapalestina litakalohakikisha usalama wa Israel. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema chama cha Hamas si mshirika wa upatanishi na nchi za magharibi, wazo ambalo limeungwa mkono na waziri wa kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice.

Waziri mkuu wa mamlaka ya Palestina, Salam Fayad, ametoa shukuranizake kwa msaada ulioahidiwa Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi. Amesema litakuwa mojawapo ya malengo ya serikali yake kuhakikisha kuna usalama zaidi wa raia. Hata hivyo amesema bilaushirikiano wa Israel, itakuwa vigumu kulifikia lengo hilo kikamilifu.

´Hii pia inahitaji ushirikiano katika maswala ya usalama kutoka upande wa Israel. Kuvipa vikosi vya Palestina uhuru wa kufanya kazi yake na wala sio kuzifuja juhudi au uwezo wa vikosi hivyo machoni pa raia´

Waziri mkuu Fayad ameitaka Israel iachane na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina, kuondoa vizuizi vya barabarani na kuwapa Wapalestina uhuru wa kutembea.

Lakini waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel, Tzipi Livini akijibu maombi hayo amesema, ´Tunataka kufanya hivyo lakini hatimaye lazima tuchague kati ya kuzifunga barabara na usalama wetu. Ili mradi kuna vyombo vya sheria upande wa Palestina, itakuwa rahisi kwetu kupitisha maamuzi lakini tuna shida ya kuyatekeleza kwa sababu ya usalama wa Israel.´

Kwenye mkutano huo wa Berlin mjumbe maalamu katika mgogoro wa Mashariki ya Kati, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair, amesema kuna ufanisi uliopatikana katika mchakato wa kutafuta amani ya eneo hilo, wazo ambalo halikuungwa mkono na katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu, Amr Musa.

 • Tarehe 01.07.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQBE
 • Tarehe 01.07.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQBE
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com