Wabunge waunga mkono uchaguzi wa mapema Uingereza | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wabunge waunga mkono uchaguzi wa mapema Uingereza

Bunge la Uingereza limepitisha kwa kura 522 dhidi ya 13 kuunga mkono mipango ya Waziri Mkuu May ya kuandaa uchaguzi mkuu wa mapema kabla ya kuanza kwa majadiliano ya Brexit.

Umoja wa Ulaya nao umesema majadiliano "kamili ya kisiasa" juu ya Uingereza kujiondoa yataanza baada ya uchaguzi wa mapema wa mwezi Juni. 

Awali Uingereza ilipanga kufanya uchaguzi wa kitaifa mwaka 2020 lakini May alisema jana Jumanne kwamba uchaguzi huo utafanyika Juni 8 mwaka huu ili kuimarisha uwezo wake katika majadiliano ya Brexit na Umoja wa Ulaya.

Katika mjadala bungeni mapema leo mchana Waziri Mkuu May alikabiliana na maswali na hoja mbalimbali kutoka kwa wabunge, ikiwemo kwa nini hataki kushiriki katika mdahalo wa Televisheni na kuzungumzia masuala hayo kwa uwazi. "Napenda kumhakikishia mheshimiwa kwamba nitajadili masuala haya kwa uwazi nchini kote na kila mwanachama wa timu ya Conservative. Tutachukua rekodi ya kujivunia ya serikali ya Conservative lakini zaidi ya hilo tutaweka mipango yetu kwa ajili ya mustakabali wa nchi hii na kuifanya Brexit kuwa mafanikio na kuifanya Uingereza kuwa imara," alisema May.

Großbritannien Brexit, House of Commons - Jeremy Corbyn, Labour Party (picture-alliance/PA Wire/empics)

Jeremy Corbyn, kiongozi wa chama cha Labour Uingereza

Wakati hayo yakijiri msemaji wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Margaritis Schinas amesema majadiliano yalikuwa yaanze mwezi Juni hata kabla ya bosi wake Jean-Claue Juncker kuzungumza na waziri mkuu May jana Jumanne.

May alizindua mchakato wa talaka ya Brexit mwishoni mwa mwezi Machi pale alipochokoza kipengele cha 50 cha mkataba wa Umoja wa Ulaya cha Lisbon. Katika hali isiyotarajiwa, siku ya Jumanne waziri Mkuu huyo alitangaza kufanyika kwa uchaguzi wa mapema wakati akijaribu kutafuta uungwaji mkono dhidi ya wapinzani kabla ya majadiliano magumu ya Brexit.

Schinas na maafisa wengine wa Umoja wa Ulaya wamesema wanatarajia kwamba azimio la mwongozo wa Brexit litakubaliwa na viongozi wa mataifa mengine 27 katika mkutano wa kilele wa hapo Aprili 29. Mawaziri kutoka nchi nyingine wanachama wamepangwa kukutana Mei 22 ili kutoa rasmi maelekezo ya majadiliano ya Brexit yatakayoongozwa na Michel Barnier ambaye awali aliwahi kushika wadhifa wa juu katika serikali ya Ufaransa.

Schinas pia anasema taasisi mbili za Umoja wa Ulaya zenye makao makuu yake Uingereza, Mamlaka ya Benki ya Ulaya na Mamlaka ya Madawa "zitahitajika kuwepo ndani ya Umoja wa Ulaya" pindi mchakato wa Brexit utakapokamilika na kwamba serikali ya Uingereza haitakuwa na "usemi" juu ya hilo kwasababu haitakuwa tena sehemu ya majailiano ya Brexit .

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters/AFP/DPA

Mhariri: Josephat Charo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com