Von der Leyen ashauri Mageuzi Jeshini | Magazetini | DW | 13.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Von der Leyen ashauri Mageuzi Jeshini

Shauri la waziri wa ulinzi la kulijongeza jeshi la Shirikisho Bundeswehr karibu zaidi na familia,na nafasi ya kufanikiwa juhudi za waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier katika jukwa la kimataifa

Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen akizungumza na wanajeshi january tisa iliyopita mjini Hannover

Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen akizungumza na wanajeshi january tisa iliyopita mjini Hannover

Tuanzie Berlin ambako pendekezo la waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen la kulifanyia marekebisho jeshi la shirikisho Bundeswehr linasifiwa na wengi wa wahariri wa magazeti ya Ujerumani.Mhariri wa "Berliner Morgenpost" anahisi:"Akifanikiwa,basi hata kansela ataweza kuwa.Ursula von der Leyen aliyetaka kwa kila hali kuwa waziri wa ulinzi,amejiwekea lengo la aina pekee:Anataka kuligeuza jeshi la Shirikisho Bundeswehr liwe la kimambo leo,na mwajiri wa kuvutia.Hapo waziri huyo wa zamani wa familia anafikiria moja kwa moja kulijongeza jeshi karibu zaidi na familia.Yote hayo ni sawa na muhimu pia.Kutokana na kutolazimika tena watu kutumikia jeshini,Ujerumani inakumbwa na shida ya kuwapata wanajeshi wanaofaa.Na katika mpango wa mageuzi unaolenga kuvifanya vikosi vya wanajeshi viwajibike zaidi,suala la kuijongeza familia karibu zaidi na jeshi halikuzingatiwa.Von der Leyen lakini analizusha hivi sasa tena kwa werevu mkubwa kupita kiasi:Pendekezo lake hakulifungamanisha na madai ya fedha."

Madai ya Wanajeshio Yazingatiwa

Gazeti la "Landeszeitung" linakumbusha:"Ukakamavu wa Ursula von der Leyen unajulikana na malengo yake makubwa makubwa pia.Mambo yote hayo mawili yanasifiwa sawa na yanavyohofiwa.Hivi sasa anataka kuligeuza jeshi la shirikisho liwe mwajiri wa kuvutia.Anataka pawepo uwiano kati ya shughuli za wanajeshi na familia .Ukweli lakini ni kwamba malengo hayo yana mipaka.Wanajeshi hawatoweza kupunguza muda wa shughuli zao wanapokuwa nchi za nje.Na hata miongoni mwa wanamaji itakuwa shida ,wanapokuwa baharini kuigeuza dira ili kurejea nyumbani kidogo kuziona familia zao.Lakini von der Leyen anapigania mengine zaidi -yale ambayo wanajeshi wamekuwa kwa muda mrefu wakiyakosoa.Na hapo anaweza kufanikiwa."

Matumaini ya Wana Social Democratic

Treffen der Gruppe der Freunde Syriens

Waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier (kati) akizungukwa kutoka kushoto na mkuu wa upande wa upinzani wa Syria Ahmad Jarba,waziri mwenzake wa Ufaransa Laurent Fabius waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Nabil Fahmy na waziri mwenzake wa Marekani John Kerry

Ripoti ya mwisho magazetini inahusu nafasi ya waziri wa mambo ya nchi za nje Frank Walter Steinemeier ya kuweza kunawiri katika jukwaa la kimataifa.Gazeti la "Der Tagesspiegel" linaandika:"Steinmeier anaweza sana kufanikiwa.Anazungukwa na kundi la wajuzi ambao hawajawahi kushuhudiwa tangu mwongo mmoja uliopita;anawajua wengi wa mawaziri wenzake wa dunia na anaudhibiti wadhifa wake ipasavyo.Na ya kale pia hajayasahau.Sio yote yalivutia alipoondoka wakati ule.Kwa hivyo pindi Steinemeier akifanikiwa safari hii,matumaini makubwa atawekewa,kwa mfano SPD watakapotaka kumchagua mgombea kiti cha kansela kwaajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inllandspresse

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman