Zelensky kuingia duru ya pili ya uchaguzi na Poroshenko
1 Aprili 2019Mratibu maalum wa shirika hilo la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE Ilkka Kanerva amewaambia waandishi habari kwamba wapiga kura nchini Ukraine walikuwa na sauti kubwa na walijitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo uliofanyika jana jumapili.
Mchekeshaji ambaye hana uzoefu wa kisiasa Volodymyr Zelensky amechukua ushindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais na kuonesha mwanzo mpya wa kisiasa kwa wapiga kura waliochoshwa na ufisadi katika taifa hilo lililoko katika msitari wa mbele likiungana na mataifa ya Magharibi kuipinga Urusi.
Huku robo tatu ya kura zikiwa tayari zimehisabiwa hii leo Volodymyr Zelensky aliye na miaka 41 ambaye anaigiza kama rais wa maigizo katika filamu maarufu katika runinga nchini humo alishinda zaidi ya asilimia 30.5 ya kura.
Hali hii inamuacha rais Petro Poroshenko kuchukua nafasi ya pili akiwa na asilimia 16.6 ya kura, pengo ambalo ni kubwa kuweza kumfikia mpinzani wake.
Poroshenko kwa sasa anakosolewa vikali nchini mwake kwa kukosa kukabiliana na ufisadi na kukosa kuimarisha hali ya maisha miaka mitano baada ya viktor Yanukovych alipoondolewa madarakani kupitia maandamano.
Waziri Mkuu wa zamani Yulia Tymoshenko amechukua nafasi ya tatu katika uchaguzi huo akiwa na asikilia 13.2 ya kura katika uwanja mkubwa wa mapambano wa wagombea 39 katika uchaguzi huu wa urais nchini Ukraine.
Duru ya pili ya uchaguzi kufanyika baada ya wiki tatu zijazo
Kwa sasa mchekeshaji Zelenskiy na Petro Poroshenko watapambana tena katika duru ya pili ya uchaguzi wiki tatu zijazo. Zelenskiy amekuwa akikosolewa kuwa na msimamo mwepesi katika masuala ya sera huku hotuba yake ya ushindi aliyoitoa hapo jana ikikosa kuelezea zaidi kile atakachokifanya baada ya kuchukua ushindi kamili.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wa Ukraine wamekuwa na maoni tofauti juu ya wagombea waliochukua ushindi wa mwazo katika duru ya kwanza ya uchaguzi. Anton mkaazi wa Kiev anasema hakutarajia mchekeshaji Volodomyr Zelenskiy kuchukua ushindi huku wengine wakisema wanaamini matokeo hayo maana kura ya maoni awali ilikuwa tayari imeshatabiri hilo.
Poroshenko, rais anayetetea kiti chake aliye na miaka 53 alimshambulia Zelenskiy akisema hayuko makini na ni chaguo baya wakati huu ambapo taifa lipo vitani na watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo