Vita vya ujangili vyaingia hatua mpya Tanzania | Matukio ya Afrika | DW | 04.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Vita vya ujangili vyaingia hatua mpya Tanzania

Baada ya serikali ya Tanzania kuwamataka raia watatu wa China wakiwa na vipande 706 vya meno ya tembo, sasa uchunguzi rasmi umeanza kubaini undani wa kadhia hiyo.

Mmoja wa askari wanyamapori akionesha pembe ya ndovu iliyokamatwa kutoka kwa majangili.

Mmoja wa askari wanyamapori akionesha pembe ya ndovu iliyokamatwa kutoka kwa majangili.

Gazeti la Mwananchi la nchi hiyo limemnukuu Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Eliezer Feleshi, akisema wanasubiri uchunguzi wa suala hilo kukamilika ili wafunguwe rasmi mashitaka.

Hata hivyo, hadi sasa kauli rasmi ya wizara inayohusika na maliasili na utalii haijapatikana na kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kulikokamatwa watu hao hapo siku ya Jumamosi, Suleiman Kova, "uchunguzi wao bado unaendelea", lakini akasita kutoa ufafanuzi hadi pale atakapopata kibali cha Balozi Khamis Kagasheki, waziri wa wizara hiyo.

Vyombo vya habari viliripoti kwamba siku ya tukio hilo, mwenyewe Balozi Kagasheki ndiye aliyeongoza operesheni ya kuwasaka watu wanaojihusisha na ujangili katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani Kinondoni sambamba na polisi na maofisa usalama na kufanikiwa kuwakamata raia watatu wa China, Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wakiwa na meno hayo.

Meno 706 ni sawa na kusema kwamba tembo 353 waliuawa katika hifadhi za wanyama pori mbalimbali za Tanzania, na hii ni miongoni mwa shehena kubwa kabisa kuwahi kukamatwa nchini humo.

"Operesheni Tokomeza" yasitishwa

Tembo kwenye mbuga za wanyama nchini Tanzania.

Tembo kwenye mbuga za wanyama nchini Tanzania.

Kukamatwa kwa raia hao Wachina kulikuja siku ile ile ambayo serikali ya Tanzania ilisitisha operesheni ya kuwasaka majangili iliyopewa jina la "Operesheni Tokomeza", kufuatia madai ya kuwepo uvunjwaji wa haki za binaadamu kulikoambatana na kampeni hiyo.

Spika wa bunge, Anna Makinda, aliliambia shirika la habari la AFP hapo Jumamosi kwamba miongoni mwa matukio yaliyoripotiwa ni kukamatwa kwa mali, kuteswa na kuuawa kwa watuhumiwa.

Polisi wa nchi hiyo wakishirikiana na maafisa wa wanyamapori walikuwa wakiwasaka watu wanaotuhumiwa kuwa majangili, huku kukiwa na ongezeko la mauaji ya tembo na vifaru katika taifa hilo la Afrika ya Mashariki, lakini nao wanatuhumiwa kufanya msako huo kibabe, ambao walikuwa wakiuwa na kukamata ovyo ovyo.

Uchunguzi wa uvunjaji wa haki za binaadamu

Tembo kwenye mbuga za wanyama nchini Tanzania.

Tembo kwenye mbuga za wanyama nchini Tanzania.

"Ilikuwa ni lazima kwa serikali kuisitisha operesheni hii kwa muda usiojulikana," alisema Makinda akiongeza kwamba uchunguzi wa kadhia hiyo utaanza rasmi wiki hii.

Balozi Kagasheki aliliambia Bunge siku ya Ijumaa kwamba operesheni hiyo aliyokuwa akiisimamia imesitishwa na kwamba "askari yeyote atakayegundulika kuhusika na matukio ya utesaji, wizi wa mali au mauaji ataadhibiwa."

Kagasheki mwenyewe aliwahi kunukuliwa muda mfupi baada ya kuanzisha kampeni hiyo kwamba askari wa wanyama pori walikuwa wameruhusiwa "kuwapiga risasi na kuwaua majangili" kama ilikuwa ni lazima kufanya hivyo.

Lakini Mbunge wa Maswa, John Shibuda, alisema bungeni siku ya Ijumaa kwamba licha ya majangili kuiathiri vibaya maliasili ya Tanzania, kuwaua wawindaji lilikuwa jambo lisilokubalika. "Maisha ya mwanaadamu ni bora zaidi kuliko ya tembo," huku wabunge wengine wakiorodhesha matukio kadhaa ya uvunjaji wa haki za binaadamu kwenye kampeni hiyo, yakiwemo mauaji.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf