1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Matumaini ya amani na hofu ya kuanza tena mapigano Iran

Bakari Ubena (dpa, ap, afp, reuters)
6 Mei 2026

Wakati kukiwa na matumaini ya kufikiwa makubaliano ya amani baina ya Marekani na Iran, Rais Donald Trump ametishia kuishambulia tena Iran ikiwa haitakubaliana na masharti yake ya kuvimaliza vita hivyo.

https://p.dw.com/p/5DNSx
Washington | Watu wakiandamana wakipinga vita vya Marekani na Iran
Watu wakiandamana mjini Washington wakipinga vita vya Marekani dhidi ya IranPicha: Mandel Ngan/AFP

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran inaweza tu kuchagua ama kukubali mpango wake wa amani au kukabiliwa na mashambulizi mapya na makubwa kuliko hapo awali.

Ujumbe huu wa Trump  umetolewa baada ya taarifa kutoka shirika la habari la Marekani Axios kuripoti kwamba Washington na Tehran zilikuwa karibu kufikia makubaliano ya kukomesha vita na kuanzisha mchakato mpana zaidi wa mazungumzo ya kina kuhusu mpango wa nyuklia ya Iran.

Hii ni baada ya Trump kutangaza kusitisha operesheni ya kijeshi ya Marekani ya kuzisindikiza meli za kibiashara zilizokwama katika Mlango-Bahari wa Hormuz, lakini akasisitiza kuwa vizuizi kwenye bandari za Iran vitaendelea.

Wakati Marekani ikisubiri jibu la Iran kuhusu pendekezo hilo la kumaliza vita, Tehran imesema inalipitia upya na itatoa maoni yake kwa mpatanishi Pakistan. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema nchi yake itaendelea kutetea maslahi yake na iko tayari kuufungua  Mlango-Bahari wa Hormuz ikiwa Marekani itaachana na vitisho vyake.

Araghchi afanya ziara mjini Beijing

Beijing | Mawaziri Wang Yi wa China akisalimiana na Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi akiwa ziarani mjini Beijing kukutana kwa mazungumzo na mwenzake wa China Wang Yi.Picha: Iranian Foreign Minister/Telegram/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alifanya ziara mjini Beijing na kukutana kwa mazungumzo na mwenzake wa China Wang Yi na kueleza kuwa walijadiliana kuhusu namna ya kuumaliza mzozo huo na Marekani, mpango wa nyuklia wa Iran pamoja na mvutano kuhusu ujia wa Hormuz huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa kuheshimu haki za Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

" Marafiki zetu wa China wanaamini pia kuwa Iran baada ya vita ni tofauti na Iran kabla ya vita, na kwamba sasa imefikia hadhi ya juu kimataifa. Imethibitisha uwezo na nguvu zake. Kwa hivyo, tunalenga kuanza awamu mpya ya ushirikiano kati ya Iran na nchi zingine," alisema Araghchi.

Rais Pezeshkian aelezea msimamo wa Iran

Teheran | Rais wa Iran Masoud Pezeshkian
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian akiwa mjini TehranPicha: Iranian Presidency/Handout/Anadolu Agency/IMAGO

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema nchi yake iko tayari kwa mazungumzo yatakayofanyika chini ya sheria za kimataifa, lakini kamwe haitakubali kulazimishwa kukubaliana na masharti ya upande mmoja yanayotolewa kwa vitisho.

Rais Pezeshkian ameitoa kauli hiyo alipozungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu Mteule wa Iraq Ali al-Zaidi. Pezeshkian ameikosoa Marekani akisema kwa upande mmoja  inaendeleza shinikizo dhidi  ya Iran  na kwa upande mwingine inatarajia kuwa Iran itajisalimisha, jambo alilosema kuwa kamwe haliwezekani.

Hayo yakiarifiwa, Mkuu wa Majeshi wa Israel amesema jeshi la nchi hiyo liko katika hali ya tahadhari na liko tayari kabisa kuanzisha tena operesheni pana na kubwa zaidi nchini Iran huku viongozi mjini Tel-Aviv wakisema kuwa hawakuwa na taarifa zozote kuhusu kukaribia kufikiwa makubaliano ya amani baina ya Marekani na Iran.