1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Vita vya Gaza: Sunak akutana na Rais wa Israel

19 Oktoba 2023

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana kwa mazungumzo na mwenzake wa Uingereza Rishi Sunak na amesema shambulio la Hamas limeharibu mpango wa upanuzi wa amani katika eneo la Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4Xlgw
Israel | Rishi Sunak in Tel Aviv
Rais wa Israel Isaac Herzog (kushoto) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak mjini Tel-Aviv, Israel (19.10.2023)Picha: Israeli GPO/Anadolu/picture alliance

Wiki kadhaa kabla ya shambulio hilo la kigaidi, Saudi Arabia na Israel walitangaza kuwa karibu kufikia makubaliano ya kurekebisha mahusiano yao, jambo ambalo lingeleta mafanikio makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati. Lakini uvamizi wa Hamas umepelekea mataifa ya kiarabu kurejea katika misimamo yao ya awali na kudhihirisha wazi kuiunga mkono Palestina.

Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ambaye yuko Tel Aviv katika ziara ya kuonyesha mshikamano na Israel amekutana kwa mazungumzo na Netanyahu na kumhakikishia uungwaji mkono katika kile Netanyahu amesema ni wakati mgumu kwa taifa hilo. Netanyahu ameutaka Ulimwengu kuwa upande wa Israel na kwa pamoja kulitokomeza kundi la Hamas alilosema ni sawa na Manazi wapya au Kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS.

Soma pia: Vikosi vya Israel vyauwa Wapalestina 7 Ukingo wa Magharibi

Mbali na kutoa kauli za kuiunga mkono Israel, Sunak ametaja pia kusikitishwa na vifo vya raia wasio na hatia katika mzozo huo:

Israel Tel Aviv Flughafen | Ankunft Rishi Sunak PM UK
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi SunakPicha: RONEN ZVULUN/REUTERS

" Sisi kama marafiki, tutashikamana nanyi, tutasimama pamoja na watu wako na pia tunataka upate ushindi. Tunatambua pia kwamba wananchi wa Palestina ni wahanga wa Hamas na ndiyo maana naupongeza uamuzi wako wa jana wa kuhakikisha njia zinafunguliwa ili misaada iweze kuingia Gaza."

Wakati vita vikiendelea, Jeshi la Israel limesema takriban watu 203 walipelekwa Ukanda wa Gaza na wapiganaji wa Hamas. Hapo awali, jeshi la Israel lilifanya makadirio ya mateka 199. Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Hamas liliua zaidi ya watu 1,400 nchini Israel mnamo Oktoba 7, na kuwateka nyara watu wengi wakati wa shambulio hilo.

Soma pia: Israel yashambulia kusini kwa Gaza

Hamas imeainishwa kama shirika la kigaidi na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na nchi nyingine kadhaa. Siku ya Jumatatu, msemaji wa kijeshi wa kundi la Hamas Abu Obaida alisema kundi hilo linawashikilia watu wasiopungua 200, huku wengine 50 wakishikiliwa na "makundi mengine", Alidai kuwa mateka 22 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza.

Mawaziri wa Ujerumani ziarani Mashariki ya Kati

Deutschland | Konflikt im Sudan | Treffen des Krisenstabs der Bundesregierung
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius (kushoto) akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Michele Tantussi/REUTERS

Wizara ya Ulinzi ya Israel imepokea leo hii shehena ya magari ya kivita kutoka Marekani na yatasawazisha magari ya jeshi la Israel yaliyoharibiwa katika mapigano na wanamgambo wa Hamas.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amewasili Tel Aviv leo Alhamisi ili kudhihirisha mshikamano kwa Israel na kufanya pia majadiliano kuhusu ushirikiano wa kijeshi. Pistorius anatarajiwa kukutana na Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant na wanatazamiwa kujadili kuhusu msaada wa vifaa vya matibabu vilivyoombwa na jeshi la Israel.

Naye Waziri wa Mambo ya  Nje wa  Ujerumani  Annalenna Baerbock amewasili mjini Amman nchini Jordan kama sehemu ya ziara yake ya kidiplomasia huko Mashariki ya Kati na anatarajiwa kukutana na mwenzake Ayman Safadi ili kuujadili mzozo kati ya Israel na kundi la Hamas unaondelea kusababisha maafa makubwa.