Viongozi wamtenga Trump katika mkutano wa G20 | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wamtenga Trump katika mkutano wa G20

Mkutano wa kilele wa G20 umeendelea kwa faragha mjini Hamburg huku kukiwa na taarifa kuwa viongozi wote wamemtenga rais wa Marekani Donald Trump kuhusu upinzani wake kwa mkataba wa mazingira wa Paris.

G20 Gipfel in Hamburg | Trump & Jinping & Merkel (Reuters/K. Nietfeld)

Kansela Angela Merkel (kulia) Xi Jimping na Donald Trump wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kilele wa G20

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo mapema leo, mwenyeji, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewatolea wito wenzake kufikia maridhiano kuhusu masuala ya biashara na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo Rais wa Marekani amejikuta peke yake, dhidi ya karibu viongozi wengine wote wanaokutana.

Bi Merkel amewakumbusha viongozi hao kuwa mamilioni ya watu kote duniani wanafuatilia kinachoendelea katika mkutano huo, wakiwa na matumaini kuwa changamoto na hofu zao zitapatiwa ufumbuzi. Amesema kundi lao linawakilisha maslahi ya eneo kubwa la dunia, na kuongeza kuwa hata wale ambao viongozi wao hawamo ndani ya chumba cha mkutano huo, wanategemea maamuzi mazuri.

''Ni sahihi kabisa kwa wale ambao hawapo hapa kutarajia kuwa tutafanya kazi nzuri. Tumejaribu ipasavyo,  na kwa upande wa Ujerumani, tumeweka agenda kuhusu masuala ya uchumi na sera zinazohusu mazingira na nishati.'' amesema Merkel na kuongeza kuwa  Ujerumani imeiangazia Afrika, kwa sababu bara hilo ni jirani ambayo Ulaya itafanya vyote iwezavyo kumsaidia kusonga mbele.

Trump asababisha utata, ajikuta akitengwa

Deutschland Hamburg - G20 - Donald Trump (Reuters/K. Nietfeld)

Sera za Rais Trump kuhusu mabadiliko ya tabianchi imemweka katika hali ya kutengwa

Bi Merkel ambaye anakabiliwa na uchaguzi mkuu mwezi Septemba, anakabiliwa na kibarua kigumu kuweza kupata muafaka katika mkutano, kuhusu masuala ya biashara, mazingira na wahamiaji, ambayo yamekuwa yenye mvutano mkubwa tangu Trump alipoingia madarakani.

Shirika la habari la China Xinhua limeripoti kuwa rais wa nchi Ji Xinping ameungana na Kansela Merkel, katika kutaka makubaliano kuhusu uhuru wa biashara, na kuzingatia ulinzi wa mazingira katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Katika tangazo lao la pamoja muda mfupi kabla ya mkutano huo kufunguliwa rasmi, viongozi wa kundi la nchi 6 zinazoinukia kiviwanda lijulikanazo kama Brics, ambazo ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, zimetaka pia kuheshimiwa kwa mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi wa Paris, ambao utawala wa Trump umeamua kutouunga mkono.

Hatimaye Putin na Trump wapeana mikono

G20 Gipfel in Hamburg | Protest & Ausschreitungen (Reuters/P. Kopczynsk)

Polisi 160 wamejeruhiwa katika makabiliano na waandamanaji

Pembezoni mwa mkutano huo, imefanyika mikutano mingine midogo kati ya viongozi wanaohudhuria, ukiwemo ule kati ya rais wa Marekani Donald Trump, na wa Urusi Vladimir Putin. Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hao kukutana ana kwa ana tangu Trump alipoingia madarakani, na mkutano wao umefuatiliwa kwa makini kutokana na sintofahamu ambayo imekuwa ikihusisha kampeni ya bwana Trump na uingiliaji kati wa Urusi katika uchaguzi uliopita nchini Marekani.

Tangu jana mkutano huu wa G20 mjini Hamburg umekumbwa na maandamano makubwa, ambayo wakati mwingine yamegeuka vurugu. Taarifa za polisi zimeeleza kuwa maafisa 160 wa polisi wamejeruhiwa, na polisi mjini humo imelazimika kuomba msaada kukabiliana na waandamanaji hao wapatao 100,000.

Shughuli iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya wake wa viongozi hao imebadilishiwa utaratibu, na mke wa rais Donald Trump Melania amelazimika kuikosa, baada ya waandamanaji kuiziba njia ambayo angeitumia kutoka hotelini kwake.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe, dw

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com