1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya waungana dhidi ya Urusi mkutano wa Maldova

Iddi Ssessanga
1 Juni 2023

Wakuu wa mataifa ya Ulaya wameonyesha umoja mbele ya uchokozi wa urusi dhidi ya Ukraine na Moldova leo Alhamisi, kwa kufanya mkutano wa kilele kwenye eneo linalobeba ajenda ya mstari wa mbele ya kisiasa ya bara hilo.

https://p.dw.com/p/4S4ly
Reublik Moldau | Europagipfel in Bulboaca | Selenskyj, Vucic, Bettel, Berset
Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Wakati mkururo mwingine wa mashambulizi ya makombora ukiilenga Kyiv, viongozi zaidi 40 kutoka kote barani Ulaya wamekutana nchini Moldova, umbali wa kilomita 20 tu kutoka mpaka tete wa taifa hilo na Ukraine iliyoharibiwa kwa vita.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alikuwa wa kwanza kuwasili, akifanya safari hiyo fupi kwa jirani yake mdogo wakati mji wake mkuu ukikadiria hasara ya usiku mwingine wa mashambulizi ya Urusi, yaliogharimu maisha ya watu watatu, akiwemo mtoto.

Rais Maia Sandu wa Moldova aliwakaribisha viongozi katika mkutano wa pili wa kilele wa Jumuiya ya kisiasa ya Ulaya mjini Bulboaca, akitumai pia kutumia fursa hiyo kuimarisha juhudi za taifa lake kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Sandu alimuambia Zelenskiy kwamba Ukraine inaiweka salama Moldova hii leo, na kuongeza kuwa wanashukuru sana kwa hilo, wakati wawili hao walipokutana kwenye zulia jekundu nje ya eneo la mvinyo la Kasri la Mimi.

Republik Moldau Gipfeltreffen der Europäischen Politischen Gemeinschaft | Maia Sandu und Wolodymyr Selenskyj
Rais Volodymyr zelenskiy (kushoto) na rais wa Moldova Maia Sandu (kulia), wakiwahili kwenye mkutano wa EPC mjini Bulboaca, Juni 1, 2023.Picha: Daniel Mihailescu/AFP/Getty Images

Kwa viongozi wengine 47 walioalikwa kujiunga nao, rais huyo alikuwa na ujumbe mwingine, akiwataka kuwekeza katika mataifa yao, kuamini katika demokrasia yao, na katika mustakabali wao wa Umoja wa Ulaya.

Zelenskiy asisitiza azma ya kujiunga na NATO

Kwa upande wake Rais Zelenskiy aliishukuru Moldova kwa kuwapokea wakimbizi wa Ukraine wakati wa vita, huku pia akizugumzia umuhimu wa Jumuiya ya Kujihami NATO kuipa Ukraine uanachama.

Soma pia: Mkutano wa viongozi wa mataifa ya Ulaya mjini Prague kutuma ishara wazi kwa Urusi

"Tunasubiri wakati NATO itapokuwa tayari kuikaribisha na kuipokea Ukraine na nadhani uhakikisho wa usalama ni muhimu sana sio tu kwa Ukraine, kwa majirani zetu wote, kwa Moldova, kwa sababu ya Urusi na uchokozi nchini Ukraine. ," alisema Zelenskiy.

Ukraine na Moldova zote zina matumani ya kuanza mazungumzo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya mwaka huu, licha ya uvamizi unaoendelea wa Moscow dhidi ya Ukraine na madai ya majaribio ya kudhoofisha mamlaka ya Moldova.

Mkutano huo wa EPC umefanyika pia umbali wa chini ya kilomita 10 kutoka mkoa uliojitenga na Moldova wa Transnistria, ambao unakaliwa na "vikosi vya kulinda amani vya Urusi."

Reublik Moldau | Europagipfel in Bulboaca | Selenskyj, Vucic, Bettel, Berset
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akizungumza na rais wa Serbia Aleksander Vucic na waziri mkuu wa Luxembourg Xavier Bettel wakati wa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya, katika kasri la Mimi mjini Bulboaca, Moldova, Juni 1, 2023.Picha: Vladislav Culiomza/REUTERS

Mkutano huo umefanyika chini ya ulinzi mkali, huku ndege za uchunguzi za NATO katika nchi jirani ya Romania zikitanua wigo wake hadi anga ya Moldova.

Mkutano huo wa kilele wa Moldova pia umejiri wakati mawaziri wa NATO, akiwemo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, wakikutana kujadili ajenda ya mkutano ujao wa kilele wa muungano huo wa kijeshi.

Soma pia: Urusi yafanya mashambulizi mapya ya anga mjini Kiev

Mkutano wa kilele wa NATO mjini Vilinius hapo Julai 11, utajadili namna ya kurasimisha ahadi ya  kuipa Kyiv uanachama na lini inaweza kujiunga na muungano huo, lakini kwa muda mfupi, Ulaya iko makini katika kuonyesha uungaji mkono.

Viongozi walikuwa wanatumia mkutano huo kama onyesho la ishara ya uungaji mkono kwa Ukraine na Moldova, wakati pia wakishughulikia masuala mengine, ikiwemo ongezeko la mzozo wa kikabila nchini Kosovo, na juhudi za kupatikana kwa amani ya kudumu kati ya Armenia na Azerbaijan.

Chanzo: Mashirika