Vifaru na ndege za Israel vyazidisha madhila Gaza
18 Septemba 2025
Mashuhuda wanasema mashambulizi ya mizinga na mabomu hayajakoma, huku familia zikilia na kuomboleza barabarani.
Shirika la Afya Duniani, WHO, limeonya kuwa maagizo ya kuhamia kusini yaliyotolewa na jeshi la Israel yamesababisha wimbi jipya la wakimbizi wa ndani, wakati hospitali zikiwa ukingoni mwa kuporomoka.
Hospitali ya Al-Shifa imeripoti kupokea miili ya watu 20 waliouawa tangu usiku wa manane, huku zaidi ya watu 60 wakipoteza maisha kwa siku moja.
Jeshi la Israel linadai kuzilenga ngome za Hamas, lakini ghadhabu ya kimataifa inaongezeka baada ya Umoja wa Mataifa kuituhumu Israel kwa mauaji ya kimbari.
Wakati huo huo, familia za mateka wa Kiisraeli walioko Gaza zilifanya maandamano mjini Jerusalem, wakimtuhumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa kushindwa kuwaokoa wapendwa wao.