1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Urusi yaishtumu Ukraine kuua raia kwa droni Kherson

2 Januari 2026

Urusi imedai zaidi ya watu 24 wameuawa katika shambulio la droni la Ukraine wakati wa sherehe za Mwaka Mpya katika eneo linalokaliwa la Kherson, huku Kyiv ikikanusha na kusema inalenga malengo ya kijeshi pekee.

https://p.dw.com/p/56DGD
Mashariki mwa Ukraine inayokaliwa na Urusi, Khorly 2026 | Athari za shambulio la droni la Ukraine dhidi ya hoteli na mgahawa
Moshi na miali ya moto baada ya shambulio la droni la Ukraine katika kijiji cha Khorly, mkoa wa Kherson, Januari 1, 2026.Picha: Vladimir Saldo/Telegram/REUTERS

Mamlaka zilizowekwa na Urusi katika eneo linalokaliwa la kusini mwa Ukraine zimedai kuwa zaidi ya watu 24 wameuawa kufuatia shambulio la droni la Ukraine lililotokea wakati wa sherehe za mkesha wa Mwaka Mpya katika kijiji cha Khorly, kilichopo kwenye mwambao wa Bahari Nyeusi.

Kiongozi wa utawala unaoungwa mkono na Urusi katika eneo la Kherson, Vladimir Saldo, alisema droni tatu zilipiga mgahawa ambako watu walikuwa wakisherehekea kuukaribisha mwaka mpya.

Saldo alisema awali watu 24 walifariki dunia lakini baadaye akaongeza kuwa idadi ya vifo ilikuwa kubwa zaidi bila kutoa takwimu mpya. Alisema pia watu wasiopungua 25 walijeruhiwa, akizungumza kupitia Telegram.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilitaja tukio hilo kuwa "shambulio la kigaidi,” ikisema kuwa takribani watu 50 walijeruhiwa, huku Rais Vladimir Putin akiarifiwa rasmi kuhusu tukio hilo.

Picha na video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mgahawa ulioteketezwa kwa moto katika kijiji hicho cha mapumziko, kilichopo takribani kilomita 70 kutoka mji wa Kherson.

Mashariki mwa Ukraine inayokaliwa na Urusi, Mkoa wa Kherson 2026 | Mkahawa ulioharibiwa baada ya shambulio la droni la Ukraine
Mkahawa ulioharibiwa baada ya shambulio la droni la UkrainePicha: Kherson Region Governor Press Of/ZUMA/picture alliance

Ukraine yakataa madai, yatetea msimamo wake

Jeshi la Ukraine limekanusha madai ya Urusi, likiyataja kama upotoshaji wa kawaida wa Kremlin unaolenga kushawishi washirika wa Kyiv na mwelekeo wa mazungumzo ya amani.

Msemaji wa Makao Makuu ya Jeshi la Ukraine alisema vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vinazingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na hushambulia malengo halali pekee.

"Vikosi vya Ulinzi vya Ukraine hushambulia malengo ya kijeshi ya adui, miundombinu ya mafuta na nishati ya Shirikisho la Urusi, na malengo mengine halali kwa lengo la kupunguza uwezo wa kijeshi wa nchi mvamizi,” msemaji huyo alinukuliwa na shirika la Interfax-Ukraine.

Baadhi ya Waukraine waamua kutoroka kuliko kupigana na Urusi

Msemaji huyo hakurejea moja kwa moja madai ya Urusi kuhusu shambulio la hoteli au mgahawa, lakini alisema mashambulizi yote ya Ukraine hutangazwa kupitia kurasa rasmi za jeshi hilo kwenye mitandao ya kijamii.

Saldo alidai kuwa mtoto alikuwa miongoni mwa waliouawa, akimtuhumu Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kukosa dhamira ya kumaliza vita.

Kherson katika mzozo wa muda mrefu wa udhibiti

Urusi ilitangaza kuikalia kinyume cha sheria mkoa wa Kherson mwaka 2022, pamoja na Zaporizhzhya, Donetsk na Luhansk, licha ya kutodhibiti kikamilifu maeneo hayo.

Udhibiti wa Kherson umegawanyika kwa mstari wa Mto Dnipro, huku vikosi vya Urusi vikishikilia sehemu ya kusini ikiwemo pwani ya Bahari Nyeusi, na Ukraine ikidhibiti sehemu ya kaskazini ikiwemo mji wa Kherson.

Baada ya tukio la Khorly, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi na wabunge wa Urusi walieleza hasira zao, huku waendesha mashtaka wakianzisha kesi za ugaidi, kwa mujibu wa shirika la habari la TASS.

Tukio hilo limeongeza mvutano wa kisiasa na kidiplomasia wakati juhudi za kimataifa za kusukuma mazungumzo ya amani zikiendelea.

Mashambulizi ya droni pande zote

Katika maendeleo mengine, Urusi imeripoti mashambulizi ya droni ya Ukraine dhidi ya miundombinu ya mafuta ndani ya Urusi, ikiwemo ghala la mafuta katika mkoa wa Kaluga.

Kituo cha kusafisha mafuta cha Ilsky kusini mwa Urusi pia kiliripotiwa kushambuliwa tena, ingawa hakukuwa na uthibitisho wa haraka kutoka kwa mamlaka rasmi.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema droni 168 za kivita za Ukraine zilidunguliwa usiku mmoja, ikionyesha kiwango kikubwa cha mashambulizi.

Meya wa Moscow Sergei Sobyanin alisema mifumo ya ulinzi wa anga ilifanikiwa kuzuia droni kadhaa zilizokuwa zikielekea mji mkuu, bila kutoa taarifa ya uharibifu wowote.

Ubunifu wa jeshi la Ujerumani wakosolewa

Ukraine nayo yaripoti mashambulizi makubwa

Kwa upande mwingine, Jeshi la Anga la Ukraine lilisema Urusi ilirusha droni 205 za kivita usiku huo huo, huku vitu 176 vya angani vikidunguliwa.

Hata hivyo, mashambulizi yalirekodiwa katika maeneo 24 ya Ukraine, huku mkoa wa Volyn kaskazini-magharibi mwa nchi ukiwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi.

Hali hii inaashiria kuendelea kwa mapigano makali karibu miaka minne tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi kamili wa Ukraine, huku pande zote zikiendelea kubadilishana mashambulizi ya droni na lawama kali za kisiasa.

Chanzo: dpae, rtre