1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yashambulia Bandari mbili muhimu za Ukraine

Amina Mjahid
16 Agosti 2023

Urusi imetumia ndege zake zisizokuwa na rubani kuishambulia upya Ukraine, kwa kuzilenga bandari za nchi hiyo jirani zilizoko kwenye mto Danube, karibu na mpaka wa Romania.

https://p.dw.com/p/4VE8a
Ghala la nafaka lililoharibiwa katika bandari iliyoko Odessa, Ukraine
Ghala la nafaka lililohaibiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na Urusi karibu na mji wa Odessa nchini Ukraine Picha: Odesa Regional Administration Press Office/AP/picture alliance

Bila ya kutaja eneo hasa lililoathiriwa kwa mashambulizi hayo, ofisi ya utawala wa mkoa wa Odessa ilisema mabohari na maghala ya nafaka yaliharibiwa vibaya katika moja ya Bandari zilizoshambuliwa. Ukraine ina bandari mbili katika mto Danube, Reni na Izmail. Picha zinazoendelea kuonekana katika mitandao ya kijamii zinaonyesha jinsi Bandari ya Reni ilivyoshambuliwa.

Ujerumani yasisitiza kuendelea kutoa misaada Ukraine

Kupitia Telegram Gavana Oleh Kiper alisema moto mkubwa uliozuka baada ya mashambulizi ulifanikiwa kuzimwa, akisisitiza kuwa hakuna aliyeuwawa au kujeruhiwa katika mkasa huo.

Kulingana na jeshi la anga la Ukraine, droni 13 za kivita zinazoaminika kutengenezwa na Iran zilidunguliwa usiku wa kuamkia leo katika miji ya Odessa na Mykolaiv iliyoko kusini mwa taifa hilo. Urusi imekuwa ikizuia usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine kupitia Odessa na bandari nyengine za Bahari Nyeusi kuanzia katikati ya mwezi Julai, kufuatia Moscow kujiondoa katika makubaliano ya kimataifa ya usafirishaji nafaka za Ukraine.

Urusi nayo yasema Imedugua droni tatu za Ukraine

Droni ya Ukraine aina ya `Punisher´
Droni aina ya "Punisher" iliyotengenezwa na kampuni ya Ukraine ya UA Dynamics ikirushwa hewani mjini KievPicha: SERGEI SUPINSKY/AFP

Kwa upande mwengine Urusi , kupitia wizara yake ya ulinzi hii leo nayo pia imetangaza kwamba imedungua droni tatu kutoka Ukraine kusini Magharibi mwa Moscow ikiwa ni tukio la hivi karibuni la mashambulizi ya angani yanayovurumishwa kutoka Ukraine.

Rais Zelenskiy autembelea mkoa wa kusini kuwaona makamanda

Wizara hiyo imesema Ukraine ilirusha makombora hayo hii leo alfajiri katika eneo la Kaluga. Gavana wa eneo hilo Vladislav Shapsha  amesema bado hapakuwa na athari yoyote kwenye miundombinu au watu wake.

Tarehe 30 mwezi Julai rais wa Ukraine  Volodymyr Zelensky alionya kwamba vita sasa vinaelekea nchini Urusi vikilenga maeneo muhimu pamoja na makambi ya kijeshi.

Ukraine yafanikiwa kukidhibiti tena kijiji cha Urozhaine

Huku hayo yakiarifiwa Jeshi la Ukraine limesema wanajeshi wake wamefanikiwa kukidhibiti kijiji cha Urozhaine, kilichokuwa kikipiganiwa kwa siku kadhaa wakati wa kujibu mashambulizi dhidi ya Urusi upande wa Mashariki.

Wanajeshi wa Urusi wakiwa mafunzoni Donetsk
Wanajeshi wa Ukraine wakiwa mafunzoni mjini Donetsk katika kambi ya Druzhkivka.Picha: Mathias Bölinger/DW

Urozhaine ipo karibu na kijiji kingine cha Staromaiorske, kilichodhibitiwa tena na Ukraine takriban wiki mbili zilizopita.

Taarifa za kukidhibiti tena kijiji hicho zimekuja siku moja baada ya waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu kusema kwamba jeshi la Ukraine limeelemewa licha ya kupokea msaada wa silaha kutoka kwa washirika wake wa Magharibi.

Vikosi vya Ukraine vinasonga mbele Bakhmut

Wakati uo huo Wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema Urusi sasa inatumia ndege zisizokuwa na rubani ilizozitengeneza yenyewe kuendelea kuishambulia Ukraine.

Ndege hizo zinasemekana kuwa na muundo kama ule wa droni za Iran.

Chanzo: Amina Abubakar/afp/ap