1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi kupeleka mfumo unaofyatua makombora ya nyuklia Belarus

John Juma
26 Juni 2022

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameahidi kupeleka mifumo ya Iskander-M inayoweza kufyatua makombora ya nyuklia nchini Belarus. Haya yamejiri mnamo wakati vikosi vya Urusi vimechukua udhibiti kamili wa mji wa Sieverodonetsk.

https://p.dw.com/p/4DFcK
Russland | Militärfahrzeug mit Iskander-M Rakete
Picha: Russian Look/picture alliance

Urusi inanuia kupeleka mifumo kwa jina Iskander-M inayoweza kufyatua makombora ya nyuklia nchini Belarus katika miezi michache ijayo. Rais Vladimir Putin alisema hayo Jumamosi kupitia televisheni ya Urusi wakati wa kuanza kwa mkutano kati yake na kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko mjini Saint Petersburg.

Putin alisema pia Urusi itaisaidia Belarus kuboresha ndege zake za kivita aina ya Su-25 kuziwezesha kubeba silaha za nyuklia.

Rais wa Belarus Lukashenko alielezea wasiwasi wake kuhusu kile alichokiita uchokozi na será za kuudhi za majirani zake Lithuania na Poland.

Alimuomba Putin kuisaidia Belarus kuwa na ‘majibu yanayofanana' na kile alichosema kuwa ndege za kivita za nyuklia zinazoongozwa na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, karibu na mpaka wa Belarus.

EU yazipa Ukraine na Moldova hadhi ya wagombea kujiunga

Putin alisema haoni sababu ya kuwa na majibu yanayofanana lakini ndege za kivita za Belarus zilizotengenezwa Urusi chapa Su-25 zinaweza kuimarishwa zaidi kukihitajika kwenye viwanda vya Urusi

Mfumo wa makombora Iskander-M ambao NATO huuita SS-26, ulichukua mahala pa ‘Scud'. Huweza kufyatua kombora umbali wa kilomita 500 na huweza kubeba zana za vita au vichwa vya nyuklia.

Urusi yachukua udhibiti kamili wa Sieverodonetsk

Kuudhibiti mji wa Sieverodonetsk uliokuwa nyumbani kwa zaidi ya wakaazi 100,000, ni ushindi mkubwa kwa Urusi tangu walipokamata bandari ya Mariupol mwezi uliopita.
Kuudhibiti mji wa Sieverodonetsk uliokuwa nyumbani kwa zaidi ya wakaazi 100,000, ni ushindi mkubwa kwa Urusi tangu walipokamata bandari ya Mariupol mwezi uliopita.Picha: Alexander Ermochenko/Reuters

Vikosi vya urusi vimechukua udhibiti kamili wa mji wa Sieverodonetsk ulioko mashariki mwa Ukraine. Pande zote mbili zimethibitisha hayo, ikiwa ni pigo kubwa kwa Ukraine kwenye mapambano makali ya zaidi ya mwezi mmoja kuupigania mji huo wa kimkakati.

Ni hatua inayobadilisha uwanja wa mapambano mashariki mwa Ukraine baada ya wiki kadhaa ambapo uwezo wa kijeshi wa Urusi ulikuwa umeleta matokeo kidogo tu.

 Ukraine imesema kuondoka kwaokatika mji huo ni hatua ya kimkakati ili kupigana wakiwa eneo ambalo limeinuka mjini Lysychansk ulioko ukingo wa upande mwingine wa mto Siverskyi Donets.

 Urusi imesema inalenga kusonga mbele kukamata maeneo zaidi katika ukingo ulioko mkabala, huku Ukraine ikitumai maafa ambayo Urusi ilipata katika mapambano ya kukamata SIeverodonetsk, yamevidhoofisha vikosi vyake na kuviweka katika hatari ya kushambuliwa. 

 Hayo yakijiri wanaotaka kujitenga na Ukraine na wanaounga mkono Urusi, wamesema vikosi vya Moscow sasa vinashambulia Lysychansk.

Zelensky aahidi kurejesha miji iliyochukuliwa na Urusi

Zelensky akiri kuwa maafa yanayotokana na vita hivyo kuwa pigo hata kihisia.
Zelensky akiri kuwa maafa yanayotokana na vita hivyo kuwa pigo hata kihisia.Picha: Natacha Pisarenko/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameapa kwamba Ukraine itairudisha miji ambayo imechukuliwa mikononi mwao ukiwemo mji wa Sieverodonetsk.

Ukraine yataka Urusi iwekewe vikwazo zaidi

 Kwenye hotuba yake kwa njia ya video, Zelensky amekiri kuwa maafa yanayotokana na vita hivyo kuwa pigo hata kihisia. "Hatujui vita vitadumu kwa muda gani, wala mapigo mangapi tutapata, juhudi zitahitajika kabla ushindi upatikane.”

 "Mji sasa upo chini ya udhibiti kamili wa Urusi,” amesema meya wa Sievierodonetsk Oleksandr Stryuk kwenye runinga ya kitaifa. "Sasa wanajaribu kuweka utaratibu wao wenyewe kusimamia mji huo, ninajua kwamba wameshaweka kamandi ya aina fulani.”

Kyrylo Budanov, mkuu wa idara ya intelijensia ya Ukraine ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Ukraine inachukua hatua ya kimkakati ambayo ni kujikusanya na kuviondoa vikosi vyake Sieverodonetsk.

"Urusi inatumia mbinu iliyotumia Mariupol, kuuharibu mji kabisa,” amesema kufuatia hali ilivyo sasa, kuendelea kupambana kwenye mahame yaliyoharibiwa ya mji huo hakuwezekani tena. Kwa hivyo vikosi vya Ukraine vinaondoka kuelekea maeneo ya juu ili kuendelea na operesheni yao ya ulinzi.

(RTRE)