1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wakaidi marufuku ya polisi kufanya mikutano Uganda

22 Mei 2024

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi pamoja na wafuasi wake wamekaidi jaribio la vyombo vya usalama la kuzuia awamu ya pili ya mikutano yao ya kisiasa katika kanda ya mashariki mwa nchi.

https://p.dw.com/p/4g9oQ
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu, anayejulikana kama Bobi Wine katika mkutano wa kisiasa.
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu, anayejulikana kama Bobi Wine katika mkutano wa kisiasa.Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Licha ya polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi na kufyetuwa risasi angani kuwasambaratisha Bobi Wine na umati  wa wafuasi wake, wamendelea kutoa shinikizo na kwamba ratiba  yao itaendelea kama ilivyopangwa.

Vurugu zimetokea kwenye daraja kuu linalounganisha kanda ya Buganda na ile ya Busoga. Polisi walijaribu kuzuia msafara wa Bobi Wine na wafuasi wake kwa kufyatua mabomu ya kutoa machozipamoja na risasi angani ili kuwasambaratisha. Ila wafuasi hao walistahimili na kulazimisha safari yao kuendelea

Chama kikuu cha Kisiasa NUP kilitangaza ratiba yao ya kuanza awamu ya pili ya mikutano yao ya kisiasa kote nchini na hii leo ndiyo ilikuwa siku ya mkutano wa kwanza mjini Kamuli kilomita 140 hivi kutoka Kampala.

Rekodi za onyo la polisi katika kushiriki maandamano

Uganda Kampala |  Kukamatwa kwa mwanasiasa Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine.
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu akiziuliwa na polisi wa kutuliza ghasia wakati wa maandamano ya kuipinga serikali huko Kampala, Uganda Machi 15, 2021.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Siku ya jumatatu msemaji wa polisi Fred Enanga aliwambia wanahabari kuwa mikutano ya chama hicho ilipigwa marufuku mwaka uliopita baada ya awamu ya kwanza ya mzunguko wa kitaifa. Hii ilitokana na viongozi wa chama hicho kukaidi maelekezo waliopewa na badala yake wakatumia mikutano hiyo kutoa matamshi ya chuki dhidi ya rais Yoweri Museveni.

Lakini kabla ya kuanza safari kwenye makao makuu ya chama hicho,rais wa NUP Robert yaani Bobi Winealiwambia wanahabari kwamba polisi haikuwa imewasiliana nao rasmi kuhusu marufuku hiyo na wana haki kama vyama vingine vya kisiasa kuendesha mikutano ya hadhara.

Zaidi alisema "Tuliwasilisha ratiba ya mikutano yetu kwa polisi siku nyingi zilizopita na sidhani tunafanya mikutano hii kinyume na sheria kwa sababu chama chetu ni chama rasmi kama vingine ambavyo vinaendesha mikutano kama hiyo."

Kamata kamata ya polisi kwa waandamanaji

Asubuhi ya leo (22.05.2024) askari wa vyombo vya usalama walizuia maandalizi mahali ambapo mkutano wa ufunguzi ungefanyika. Waliwazuia wahudumu kukita mahema na kuandaa vipaza sauti huku watu kadhaa ikiwemo wafuasi na wanahabari wakikamatwa. Lakini wafuasi wa NUP wamesisitiza kuwa hawatatishiwa kuendelea na mikutano yao.

Chanzo:Zoezi la sensa Uganda laanza na malalamiko ya wafanyakazi

Polisi na vyombo vingine vya usalama wanaelezea kuwa wanatekeleza sheria ya mikusanyiko na mikutano inayowataka wandalizi kuwasilisha taarifa za kufanya mikutano yao siku 15 kabla ya mikutano hiyo kufanyika. Lengo ni kulinda watu wengine wasitatizwe kuendesha shughuli zao pamoja na kuakikisha uthabiti. 

DW Kampala.