1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Kongo na Uganda yawauwa wanamgambo watano Beni

John Kanyunyu26 Aprili 2024

Vikosi vya operesheni ya pamoja ya jeshi la Uganda UPDF na lile la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo FARDC, vimewaua wapiganaji watano wa kundi la waasi la ADF na kuwateka nyara wangine wanne.

https://p.dw.com/p/4fDGD
Kongo | Soldaten in Beni, DRC
Picha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Akizungumza na waandishi habari katika mji mdogo wa Mavivi/Ngite, msemaji wa jeshi la Kongo kwenye eneo la Kivu kaskazini Kapteni Anthony Mualushayi amesema kazi kubwa imefanywa na vikosi vya operesheni ya pamoja katika mji mdogo wa Mavivi/Ngite, ambapo walifanikiwa kuwaua magaidi watano wa ADF.

"Tumewauwa magaidi wa ADF/MTM watano. Mateka mmoja kwa jina la Bizimaana Sobomana mzaliwa wa wilaya ya Masisi, tunae bwana Ngahangondi Jean-Paul anayejulikana sana hapa kwani alikuwa mbunge, lakini cha kushangaza tulimkuta katika mashambulizi wakati mmoja, yeye akiwa upandewa wa ADF'', alisema Mwalushayi.

''Nilisikia milio nyingi ya risasi''

Na akiwa miongoni mwa mateka waliooneshwa kwa waandishi wa habari, mbunge wa zamani wa jimbo kwa awamu iliyopita na akiwa pia mwanaharakati wa haki za binadamu Jean-Paul Ngahangondi, alikanusha tuhuma za jeshi dhidi yake akisema, kwamba alikuwa akitokea mjini Beni kikazi na kwenda kwenye mji wa Oicha.

Kwa bahati mbaya akajikuta katika eneo la mapambano na ndio alipojaribu kukimbia, alianguka kwenye pikipiki na hapo ndipo wanajeshi walimkamata na kumpeleka mahali palipo na usalama.

''Nilisikia milio nyingi ya risasi, na nikajaribu kugeuza pikipiki yangu bahati mbaya nilianguka na baade wanajeshi wa FARDC na UPDF walinikuta mahala hapo.'', alijitetea Ngahangondi ambaye ametuhumiwa kushirikiana na waasi wa ADF. 

Wito kwa raia kubaki watulivu

Jeshi la Uganda limeshiriki katika operesheni ya pamoja na jeshi la Kongo dhidi ya waasi wa ADF
Jeshi la Uganda limeshiriki katika operesheni ya pamoja na jeshi la Kongo dhidi ya waasi wa ADFPicha: AFP

Naye kamanda wa kikosi cha jeshi la Uganda UPDF kilichokabiliana na waasi wa ADF, Tembo Mike, anaelezea mazingira aliyopatikana mbunge huyo wakati wa mapambano.

''Atakabidhiwa viongozi ili wamchunguze zaidi, kwa sababu eneo alipokuwa ndipo adui ametokea.''

Wakaazi wa Mavivi siku hizi wanaishi katika hali ya wasiwasi, kufuatia mashambulizi ya ADF kila siku, na chifu wa jamii ya Batangi/Mbau Augustin Kapupa amewataka raia kuwa watulivu kwani jeshi linachapa kazi vizuri na kwamba muda si mrefu eneo lao litakuwa salama.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, wanamgambo wa ADF wamezidisha mauwaji katika maeneo ya magharibi mwa Beni, na watu wasiopungua sitini waliuawa katika kipindi cha mwezi moja uliopita. John Kanyunyu DW, Beni.