1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Raia milioni 4.9 wa Ukraine wameikimbia nchi hiyo

18 Aprili 2022

Umoja wa Mataifa umesema leo kuwa zaidi ya raia milioni 4.9 wa Ukraine wameikimbia nchi yao kufuatia uvamizi wa Urusi na kuonya juu ya hatari ya kunyanyaswa kingono kwa wakimbizi wanawake na watoto.

https://p.dw.com/p/4A4Uw
Ukraine Lwiw | Flüchtlinge auf dem Weg Richtung Polen
Picha: Joe Raedle/Getty Images

Umoja wa Mataifa umesema leo kuwa zaidi ya raia milioni 4.9 wa Ukraine wameikimbia nchi yao kufuatia uvamizi wa Urusi na kuonya juu ya hatari ya kunyanyaswa kingono kwa wakimbizi wanawake na watoto ama kuwa wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR, limesema raia wa Ukraine 4,934,415 wameikimbia nchi hiyo tangu Urusi ilipoivamia mnamo Februari 24, idadi hiyo ya leo ikiwa ni ongezeko la watu wengine 65,396 tofauti na idadi iliyotolewa jana Jumapili.

Soma pia: Pasaka yaadhimishwa Ukraine ikizidi kushambuliwa

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM), limesema karibu watu 215,000 kutoka mataifa mengine waliokuwa wakiishi Ukraine, wengi wao wanafunzi na wafanyikazi wa kigeni, pia wamekimbilia usalama wao katika nchi jirani ikimaanisha kuwa zaidi ya watu milioni tano wameikimbia Ukraine tangu kuanza kwa vita.

Hali hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa janga kubwa la kibinadamu kuwahi kutokea.

Wanawake na watoto wanajumuisha asilimia 90 ya waliotoroka.

Polen - Geflüchtete aus der Ukraine
Wakimbizi wakiwemo watoto wakiwasili katika mpaka wa Medyka, Poland.Picha: Amy Katz/ZUMA Press Wire/picture alliance

Wanawake na watoto wanajumuisha asilimia 90 ya waliotoroka vita vya Ukraine, huku wanaume wenye umri wa miaka 18 hadi 60 wakisalia nchini humo ili kulisaidia jeshi la Ukraine katika mapambano yake dhidi ya vikosi vya Urusi.

Takriban theluthi mbili ya watoto wa Ukraine wamelazimika kuondoka majumbani mwao, wakiwemo wale ambao bado wamesalia nchini humo.

"Wakimbizi kutoka Ukraine, idadi kubwa ikiwa ni wanawake na watoto, wanakabiliwa na hatari ya kunyanyaswa kingono, ama kuwa wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu,” UNHCR imesema.

"Tuko katika maeneo ya tukio na mipakani, na tunachukua hatua kuzuia hali hiyo kutokea.”

Zaidi ya wakimbizi milioni 2.75 raia wa Ukraine wamekimbilia nchini Poland, wakati wengine wapatao 740,000 wamewasili Romania.

Soma pia:Njia zaidi za kiutu zaundwa Ukraine

Takwimu za UNHCR zinaonyesha kuwa karibu Waukraine 645,000 wameikimbia nchi hiyo tangu Februari, huku wengine milioni 3.4 wakiimbia nchi hiyo mnamo mwezi Machi na karibu 900,000 wakiondoka mwezi huu wa Aprili.

Kando na hao wakimbizi, Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji linakadiria kuwa watu milioni 7.1 wameyakimbia makaazi yao lakini bado wamesalia nchini Ukraine.

Kabla ya uvamizi huo, Ukraine ilikuwa na idadi ya watu milioni 37 chini ya maeneo yanayodhibitiwa na serikali, ukiondoa eneo la Crimea linalotawaliwa kimabavu na Urusi pamoja na maeneo mengine ya mashariki yanayodhibitiwa na makundi ya wapiganaji yanayoungwa mkono na Urusi.

Maelfu ya watu wamekimbilia mataifa jirani kutafuta hifadhi.

Rumänien Luxushotel in Suceava
Wakimbizi wa Ukraine wakiwa ndani ya hoteli ya kifahari ya Mandachi iliyogeuzwa kuwa sehemu ya kupokea wakimbizi.Picha: Alessandro Serrano/Photoshot/picture alliance

Kulingana na UNHCR, takriban wakimbizi 6 kati ya 10 wa Ukraine, ambao ni watu 2,780,913 wameingia nchini Poland.

Jumla ya Waukraine 743,880 wamekimbilia katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, ikiwemo idadi kubwa walioingia Moldova, iliyoko kati ya Romania na Ukraine. Wengine wanadhaniwa huenda wamekwenda kutafuta hifadhi katika mataifa mengine.

UNHCR imesema wakimbizi 522,404 wametafuta hifadhi nchini Urusi.

Wakimbizi 105,000 wamevuka na kuingia Urusi kutoka maeneo yanayodhibitiwa na wapiganaji wanaoungwa mkono na Urusi-Donetsk na Lugansk mashariki mwa Ukraine kati ya Februari 18 na 23.

Soma pia: Ujerumani yavunjwa moyo na Ukraine

Waukraine 461,539 wameingia Hungary.

Mpaka wa Moldova ndio uko karibu Zaidi na mji mkuu wa bandari wa Odessa. Jumla ya Waukraine 423,852 wamevuka na kuingia Moldova, nchi hiyo isiyokuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya na moja kati ya mataifa maskini zaidi barani Ulaya.

Wakimbizi wengi walioingia Moldova, ambayo ni jamhuri ya zamani ya uliokuwa muungano wa Kisovieti wamehamishwa japo takriban wakimbizi 100,000 wamesalia ikiwa ni pamoja na watoto 50,000- wakati watoto 1,800 tu ndio waliojiunga na shule.

Wakimbizi wapatao 337,311 wamevuka mpaka na kuingia Slovakia wakati wengine 23,469 wakielekea upande wa kaskazini na kuingia nchini Belarus, ambaye ni mshirika wa karibu wa Urusi.