UN yatoa wito wa kupelekwa misaada zaidi Gaza
14 Oktoba 2025
Makubaliano dhaifu ya amani huko Mashariki ya Kati ambayo yalifikiwa chini ya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump yanajumuisha hatua ya kusitisha vita vya miaka miwili huko Gaza , kuachiwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa kipalestina na kuruhusu mtiririko wa misaada ya kibinaadamu katika eneo hilo linalokabiliwa na baa la njaa.
Mnamo Agosti 22, Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kuwepo kwa baa la njaa huko Gaza, ikiwa ni kwa mara ya kwanza hali hiyo kushuhudiwa huko Mashariki ya Kati, baada ya wataalam kutahadharisha kuwa watu 500,000 walikuwa katika hali mbaya zaidi.
Umoja wa Mataifa, Shirika la Msalaba Mwekundu pamoja na shirika la kimataifa la kutoa misaada ya kibinadamu OCHA wametoa wito hii leo wa kufungua vivuko vyote vinavyoelekea Gaza ili kuwezesha usambazaji wa misaada ya kibinaadamu, wakitaka pia kukarabati vivuko vilivyoharibiwa na vita. Taarifa za awali zilisema kuwa kuanzia jana, malori zaidi ya 300 yamekuwa yakiingia Gaza kupitia vivuko vya Al-Awja na Kerem Shalom.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq ameelezea umuhimu wa kufanikisha zoezi la utoaji msaada kwa Wapalestina:
" Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaongeza kasi ya operesheni za kiutu kote Gaza na kuzifikia jamii katika maeneo yaliyokuwa yamezingirwa kwa miezi kadhaa na kutoa msaada wa kuokoa maisha. Juhudi hizi zinaashiria hatua ya kwanza muhimu katika kuleta utulivu na kurejesha utu. Lakini mahitaji bado ni makubwa, hivyo ufikiaji wa maeneo hayo na ufadhili endelevu ni muhimu. "
Makubaliano hayo ya amani yapongezwa
Viongozi mbalimbali wa ulimwengu wameendelea kupongeza kufikiwa makubaliano hayo ya amani ambayo yanatoa matumaini ya kurejesha hali ya utulivu huko Mashariki ya Kati, lakini Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez licha ya kupongeza pia makubaliano hayo ya amani amesema nchi yake itaendeleza mashtaka ya uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya Israel akisisitiza kuwa amani haiwezi kufuta makosa hayo na wala haimanishi kutowawajibisha mbele ya vyombo vya sheria waliohusika wa vitendo hivyo.
Huko Gaza kwenyewe, Wapalestina wameelezea wasiwasi wao kufuatia vitendo vya mwanamgambo wa Hamas kuwauwa watu wanane hadharani pamoja na makabiliano kati ya Hamas na makundi mengine pinzani, hali inayoweza kuvuruga usalama hata baada ya kusainiwa makubaliano hayo ya amani.
// DPA, AP, RTR, AFP