Ukraine yasema wanajeshi wa Urusi wamefikia 30,000 | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ukraine yasema wanajeshi wa Urusi wamefikia 30,000

Serikali ya Ukraine imesema wanajeshi wa Urusi nchini humo sasa wamefikia 30,000 katika wakati ambapo maafisa wa Urusi wanakutana na wenzao wa mkoa wa Crimea, ambako tayari bunge limepiga kura ya kujiunga na Urusi.

Spika wa Bunge la Urusi, Valentina Matvienko (kulia), akimkaribisha mwenzake wa Crimea Vladimir Konstantinov mjini Moscow.

Spika wa Bunge la Urusi, Valentina Matvienko (kulia), akimkaribisha mwenzake wa Crimea Vladimir Konstantinov mjini Moscow.

Idadi hiyo ya wanajeshi wa Urusi katika mkoa wa Crimea, ni mara mbili zaidi ya ile iliyotolewa hivi karibuni na serikali kuu mjini Kiev. Serhiy Astakhov, mkuu wa kikosi cha kulinda mipaka, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba idadi hii inajumuisha wanajeshi walioingia kupitia nchi kavu na wale waliopitia baharini.

Hata hivyo, Urusi imekuwa ikisema kwamba wanajeshi pekee walioko huko ni wale walio kwenye kituo chake cha kijeshi cha Sevastapol, ambao wamekuwa hapo kwa makubaliano kati ya mwaka 1994 kati yake na Ukraine.

Urusi tayari kuipokea Crimea

Wanajeshi wa Urusi kwenye jimbo la Crimea, Ukraine.

Wanajeshi wa Urusi kwenye jimbo la Crimea, Ukraine.

Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Urusi, Valentina Matvienko, ametangaza hivi leo kwamba Crimea itakuwa sehemu kamili ya Urusi ikiwa wakaazi wa mkoa huo watachagua kujitenga na Ukraine kwenye kura ya maoni itakayofanyika tarehe 16 mwezi huu.

Matvienko amesema hayo baada ya kukutana na mkuu wa bunge la Crimea kujadiliana uwezekano wa mkoa huo kujiunga na Urusi.

"Ikiwa uamuzi umefanyika kupitia kura ya maoni, basi Crimea itakuwa sehemu yenye usawa kwenye Shirikisho la Urusi," alisema Matvienko, akiweka msisitizo kwenye masikitiko ya raia wanaozungumza Kirusi katika mikoa ya mashariki na kusini ya Ukraine, ambao wamekuwa hoja kuu ya Urusi kuingilia kwenye taifa hilo jirani.

Hapo jana, bunge la Crimea lilipitisha hoja ya kuisogeza karibu tarehe ya kura hiyo ya maoni na pia kuongeza swali la kujiunga na Urusi, ambalo awali halikuwemo kwenye karatasi ya kura iliyokuwa ipigwe tarehe 25 Mei mwaka huu kusadifiana na uchaguzi mkuu wa Ukraine.

Matvieko amesema hakutakuwa tena na haja ya kufanyika uchaguzi huo, kwani hakuna mazingira ya uchaguzi wa ukweli, usawa na uwazi nchini Ukraine.

Bunge la Urusi kubadilisha sheria

Wanafunzi wa Ukraine wakiunga mkono kile wanachokiita Ukraine moja dhidi ya kampeni ya Urusi kwenye mkoa wa Crimea.

Wanafunzi wa Ukraine wakiunga mkono kile wanachokiita "Ukraine moja" dhidi ya kampeni ya Urusi kwenye mkoa wa Crimea.

Jumanne iliyopita, Rais Vlamidir Putin wa Urusi aliwaambia waandishi wa habari kwamba nchi yake haikuwa na nia ya kuichukua Crimea, lakini wakaazi wa huko walikuwa wana haki ya kuamua hadhi ya baadaye ya mkoa wao, hata ikibidi uhuru kamili, kupitia kura.

Sasa kura ya maoni ya tarehe 16 Machi inawapa wakaazi hao hiyari ya kuamua tu ikiwa ama wabakie kuwa sehemu ya Ukraine au wajiunge tena na Urusi.

Kwa upande mwengine, Bunge la Urusi linajaribu kuanzisha sheria itakayorahisisha mchakato wa Crimea kujiunga na nchi hiyo. Kwa mujibu wa katiba iliyopo sasa, Urusi inaweza tu kulikubali eneo la nchi ya kigeni kuwa sehemu yake, baada ya makubaliano yatakayoanzishwa na serikali ya nchi hiyo ya kigeni.

Kwa kuwa bado kisheria Crimea ni sehemu ya Ukraine, makubaliano ya kujiunga kwake na Urusi lazima yasainiwe na utawala mpya mjini Kiev, ambao Urusi hauutambui na ambao pia unaituhumu serikali ya Moscow kwa kuingilia kijeshi kwenye ardhi yake.

Sheria hiyo mpya italiondoa sharti hilo, na kwa mujibu wa wabunge, inaweza ikapitishwa wakati wowote wiki ijayo. Ikiwa itapita, Crimea utakuwa mkoa wa kwanza kujiunga rasmi na Urusi tangu kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti hapo mwaka 1991.

Mikoa ya Ossetia ya Kusini na Abkhazia, ambayo ilijitoa kwenye taifa la Georgia baada ya vita vifupi na Urusi vya mwaka 2008, imekuwa ikitambuliwa kama nchi huru na Urusi, lakini kumekuwa na jitihada za kuiunganisha na Urusi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com