Cremea yatangaza kujiunga na Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Cremea yatangaza kujiunga na Urusi

Umoja wa Ulaya na Marekani zimetangaza hatua za mwanzo dhidi ya Urusi kuhusiana na hali inayoendelea katika eneo la Cremea nchini Ukraine, ambalo limepiga kura kujiunga na Urusi.

Viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya wakiwa katika mkutano wao mjini Brussels, Ubelgji.

Viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya wakiwa katika mkutano wao mjini Brussels, Ubelgji.

Umoja wa Ulaya ulitangaza kuwa utasisitisha mazungumzo na Urusi kuhusu utoaji wa viza, baada ya mkutano wa viongozi ulioitishwa haraka kujadili hali nchini Ukraine jana Alhamisi. Taarifa ya baraza la Ulaya ilitangaza pia kuahirishwa kwa majadiliano yanayoendelea, ambayo yalianza mwaka 2008, kuweka msingi mpana zaidi wa mahusiano katika umoja huo na Urusi, kuliko ule uliowekwa na makubaliano ya mwaka 1994. Brussels iliisihi tena Urusi kufanya majadiliano na serikali mpya mjini Kiev, ambayo Moscow imekataa kuitambua.

"Ikiwa hakutakuwa na njia za kidiplomasia, na hili lionekane si katika miezi mitatu, bali katika siku chache zijazo, basi laazima tujibu, na majibu hayo yatajumuisha hatua kadhaa zikiwemo kuzuwia mali, na kudhibiti utoaji wa viza. Lakini kabla ya yote hayo tutafanya kila tuwezalo kuupeleka mbele mchakato wa kidiplomasia," alisema Kansela Angela Merkel mjini Brussels siku ya Alhamisi.

Rais Barack Obama alizungumza na rais Putin na kumjulisha juu ya vikwazo kwa maafisa wa serikali yake.

Rais Barack Obama alizungumza na rais Putin na kumjulisha juu ya vikwazo kwa maafisa wa serikali yake.

Bunge la jimbo la Crimea linaloegemea upande wa Urusi, lilipiga kura siku ya Alhamisi, kujiunga na shirikisho la Urusi, na lilitangaza kufanyika kwa kura ya maoni katika rasi hiyo yenye wakaazi wapatao milioni mbili wiki ijayo. Kansela Merkel alisema kuwa kura hiyo ya maoni iliyopendekezwa imejengwa kwa misingi ambayo hata haipo. Muda mfupi baada ya kura hiyo ya bunge la Cremea, mji wa Sevastopol ulijitangaza kuwa sehemu ya Urusi

Waziri mkuu wa muda wa Ukraine Arseny Yatsnyuk, aliwaambia viongozi wa Ulaya kuwa yeye na wenzake mjini Kiev bado wana matumaini ya kufikiwa kwa suluhisho la kidiplomasia, lakini akaonya kuwa serikali ya Ukraine na jeshi wako tayari kulinda nchi hiyo. Viongozi wa Umoja wa Ulaya pia waliidhinisha kutolewa kwa euro bilioni 11 katika msaada wa dharura kwa Ukraine.

Obama, Putin washindwa kuafikiana

Rais wa Marekani Barack Obama, ambaye alizungumza kwa njia ya simu na rais wa Urusi Vladmir Putin kwa saa nzima, akipendekeza mazungumzo ya ana kwa ana kati ya serikali za Ukraine na Urusi kama njia ya kutatua mgogoro huo kidiplomasia, alisema kura ya maoni ya Crimea iliyopangwa kufanyika Machi 16 itakiuka katiba ya Ukraine na sheria ya kimataifa. Aliongeza kuwa mazungumzo yoyote kuhusu mustakabali wa Ukraine laazima uihusishe serikali halali ya Ukraine.

Spika wa bunge la Cremea, Vladimir Konstantinov ( wa pili kulia), na spika wa bunge la Urusi, Valentina Matviyenko ( wa tatu kushoto) wakiwa katika mkutano mjini Moscow. Bunge la Urusi limesema litaheshimu maamuzi ya watu wa Cremea.

Spika wa bunge la Cremea, Vladimir Konstantinov ( wa pili kulia), na spika wa bunge la Urusi, Valentina Matviyenko ( wa tatu kushoto) wakiwa katika mkutano mjini Moscow. Bunge la Urusi limesema litaheshimu maamuzi ya watu wa Cremea.

Ikulu ya Kremlin imesema katika taarifa kuwa rais Putin alimuambia rais Obama kuwa hatua zilizochukuliwa na Urusi nchini Ukraine hazikiuki sheria ya kimataifa. Taarifa hiyo ilisema Putin aliilaumu serikali mpya mjini Kiev wakati wa mazungumzo na Obama, akisema imetokana na mapinduzi yanayokwenda kinyume na katiba, na kusema Urusi ilishindwa kupuuza maombi ya ulinzi kutoka kwa maeneo ya mashariki na kusini yanayoegemea upande wake. Putin alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Urusi na Marekani, na kusema anatumai hautageuka mhanga wa tofuati juu ya masuala fulani.

Wakati huo, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana kwa mara ya nne wiki hii kujadili matukio ya Crimea, katika mikutano inayoitishwa na Uingereza, lakini hakuna muafaka uliofikiwa. Nalo shirika la polisi ya kimataifa Interpol, limesema kuwa linaagalia ombi la Ukraine kutoa waranti wa kukamatwa kwa rais alieondolewa Viktor Yanukovych.

Mwandishi: Bernd Riegert/DW Brussels
Iddi Ismail Ssessanga/DW,AP, dpa
Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com