Ujerumani yawasili Brazil tayari kumenyana | Michezo | DW | 09.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Ujerumani yawasili Brazil tayari kumenyana

Ujerumani ni miongoni mwa timu nyingi zilizowasili nchini Brazil kusubiri kuanza kwa dimba la Kombe la Dunia litakalofunguliwa rasmi Alhamisi Juni 12 hadi Julai 13

Vikosi vya England, Ujerumani na Uhispania viliwasili jana nchini humo huku Cameroon ambayo ikichelewesha safari yao kutokana na mgogoro wa marupurupu. England iliwasili mjini Rio De Janeiro baada ya safari ya usiku kucha kutokea Miami na ikasindikizwa na jeshi la polisi hadi hotelini mwao eneo la Sao Conrado. England, watacheza mchuano wao wa ufunguzi wa kundi D dhidi ya Italia mjini Manaus siku ya Jumamosi.

Vikosi vingine kati ya timu 32 zinazocheza dimba hilo vinaendeela kuwasili kabla ya mchuano wa kwanza wa Brazil dhidi ya Croatia mnamo Juni 12. Pamoja na wenyeji, timu 20 zimewasili nchini Brazil. Mamia ya mashabiki wameikaribisha Ujerumani wakati vijana hao wa Kocha Joachim Löw waliwasili katika mji wa Santa Cruz Cabralia, wa jimbo la kaskazini mashariki la Bahia, na wakapanda mashua kuelekea Santo Andre ambako ndiko kuna kambi yao ya “Campo Bahia” iliyojengwa maalum kwa ajili ya dimba hilo.

Deutsche Nationalmannschaft Ankunft in Brasilien WM 2014

Umati wa mashabiki uliilaki timu ya taifa ya Ujerumani "Die Mannshaft" ilipowasili Brazil

Meneja wa Kikosi cha Ujerumani Oliver Bierhoff anasema hali ya hewa kwa sasa nchini humo ni shwari na anasema kikosi kinasubiri tu shughuli yenyewe kuanza. Anasema "Naam, nadhani matarajio yako juu, kama tu inavyokuwa wakati timu ya Ujerumani inapoelekea katika Kombe la Dunia. tunafahamu kuwa sisi ni miongoni mwa wanaopigiwa upatu. kwa kweli, Brazil ndio wenye nafasi kubwa kwa sababu wanacheza nyumbani, mazingira mazuri. Hatujui mambo yatakwendaje kwa timu za Ulaya kucheza hapa lakini tumekuja hapa kuwa na dimba nzuri".

Ujerumani itacheza mchuano wake wa kwanza wa Kundi G dhidi ya Ureno mnamo Juni 16. Urusi, Ugiriki na Algeria pia zilitua nchini Brazil jana Jumapili. Timu ya Cameroon mapema jana ilisusuia kupanda ndege yao kuelekea Brazil kwa sababu ya mgogoro wa muda mrefu wa marupurupu ya wachezaji. Hali hiyo ilililazimu shirikisho la soka la kitaifa kuchukua mkopo ili kutimiza matakwa yao. Baada ya hali hiyo kutatuliwa vijana wa The Indomitable Lions kisha waliweza kuondoka mjini Yaounde mapema leo kuelekea Brazil ikiwa ni siku nne kabla ya mchuano wao wa kwanza dhidi ya Mexico siku ya Ijumaa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman