Ujerumani yapata rais mpya | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yapata rais mpya

Mwanaharakati wa zamani wa haki za binaadamu nchini Ujerumani Joachim Gauck amechaguliwa kuwa rais mpya wa Ujerumani siku ya Jumapili (18.03.2012 ).

Rais mpya wa Ujerumani Joachim Gauck

Rais mpya wa Ujerumani Joachim Gauck

Gauck amekuwa mgombea wa kwanza kutoka iliokuwa Ujerumani Mashariki kuongoza nchi, akiwekewa matumaini makubwa kwamba atarudisha heshima katika ofisi hiyo ya rais kufuatia kashfa zilizowasibu watangulizi wake wawili.

Gauck mwenye umri wa miaka 72 alijizolea kura 991 kati ya kura 1,232 kutoka kwa wabunge na watu wengine mashuhuri kutoka fani mbali mbali ikiwemo michezo,utamaduni, burudani, sayansi na dini.Mpinzani wake pekee alikuwa Beate Klarsfeld mwenye umri wa miaka 73 ambaye aliteuliwa na chama cha mrengo wa shoto cha 'Die Linke ' Gauck alikuwa akiiungwa mkono na vyama vikuu vya kisiasa nchini Ujerumani jambo ambalo lilikuwa tayari limemuhakikishia kuidhinishwa kushika wadhifa huo katika kikao cha Baraza maalum la wawakilishi wa majimbo kilichofanyika katika jengo la bunge katikati ya mji mkuu wa Berlin.

Merkel ampongeza rais mpya

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akimpongeza rais mpya

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akimpongeza rais mpya

Kansela Angela Merkel alikuja kumuunga mkono mwananchi mwenzake huyo wa Ujerumani ya Mashariki hapo mwezi wa Februari baada ya Rais Christian Wullf kujiuzulu kutokana na kuandamwa na madai ya rushwa yalioanzia hata kabla ya kushika wadhifa huo.

Wulff alitumika kwa miezi 20 tu katika muhula wake wa miaka mitano madarakani.Yeye alichukuwa nafasi hiyo kutoka kwa Horst Koehler mkuu wa zamani wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF ambaye alijiuzulu baada ya matamshi yake kuzusha shutuma kwa kuhalilisha kutumika kwa jeshi la Ujerumani kwa maslahi ya kiuchumi ya nchi hiyo.

Kurudisha imani kwa wananchi

Katika kikao cha ufunguzi msemaji wa bunge Nornert Lambert ameitaka Ujerumani ifanye juhudi za kurudi kuutumikia wadhifa wa urais kwa miaka mitano kama ilivyotajwa katika katiba. Alikuwa akimaanisha vipindi vifupi vilivyotumikiwa na Wulff na mtangulizi wake Köhler. Lambert amesema hakuna mtu ambaye atakayeona utumishi wa muda mfupi katika wadhifa huo wa urais kuwa ni mafanikio kama ilivyokuwa imeshuhudiwa hivi karibuni. Ameongeza kusema ni jambo lisilowezekana kutumikia wadhifa huo bila ya uaminifu.

Uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni ulidokeza kwamba asilimia 80 ya Wajerumani waliohujiwa walikuwa na imani naye. Gauck aliyezaliwa huko Rostock ilioko Ujerumani ya Mashariki ya zamani hana mafungamano na chama chochote kile cha kisiasa nchini sifa yake kubwa ni kutowa maoni yake bila ya woga kuhusiana na suala la uhuru. Wakati fulani aliwahi kujitambulisha kuwa ni "mhafidhina kutoka sera za kiliberali za mrengo wa shoto".

Beate Klarsfeld ni nani?

Aliyekuwa mpinzani wa Gauck, Beate Klarsfeld

Aliyekuwa mpinzani wa Gauck, Beate Klarsfeld

Mpinzani wake kwa wadhifa huo Beate Klarsfeld mwanamke aliyezaliwa Berlin aligonga vichwa vya habari hapo mwaka 1968 wakati alipomchapa kibao cha uso aliyekuwa Kansela wakati huo Kurt Georg Kiesinger mwanachama wa zamani wa chama cha Manazi wakati wa mkutano wa kisiasa wa chama hicho.

Beate aliyeteuliwa na chama cha mrengo wa shoto kuwania wadhifa huo wa urais yeye na mume wake Serge Klarsfeld ambaye baba yake Myahudi aliangamia chini ya mikono ya Manazi alitumia muda mkubwa wa maisha yao kuwaandama Manazi akiwemo Klaus Barbie anayejulikana zaidi kwa jina la 'Mchinjaji wa Lyon'

Mwezi uliopita wakati alipoteuliwa na chama cha mrengo wa shoto alisema morali yake daima ilikuwa ni kupigania kuboresha kile alichokiita 'taswira mbaya ya Wajerumani ilioko nje'

Gauck rais mteule wa Ujerumani ataapishwa katika bunge la shirikisho na baraza la wawakilishi wa majimbo hapo Ijumaa ijayo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/RTRE,DPAE,DW

Mhariri: Pendo Paul, Ndovie

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com