1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yajiandaa kwa mashambulizi ya kisasi

23 Februari 2020

Vikosi vya usalama nchini Ujerumani vinajiandaa kwa uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kulipiza kisasi kufuatia tukio la wiki hii la ufyatuaji risasi katika mji wa magharibi mwa Ujerumani Hanau.

https://p.dw.com/p/3YDt0
Deutschland Tote durch Schüsse in Hanau
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Probst

Shirika la habari la The Funke limewataja wapelelezi wa ugaidi wakisema kuwa sasa kuna uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa watu wa siasa kali za mrengo wa kushoto, pamoja na mashambulizi dhidi ya wawakilishi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany – AfD.

Duru zimeliambia shirika hilo la habari ambalo ni tatu kwa ukubwa nchini Ujerumani kuwa ijapokuwa hakuna kitisho maalum cha mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa watu wa itikadi kali, uwezekano huo hauwezi kufutiliwa mbali.

Deutschland Demonstration in Hanau nach Anschlag
Viongozi wamelaani shambulio la HanauPicha: picture-alliance/dpa/N. Armer

Jumatano usiku, Mjerumani mwenye umri wa miaka 43 aliwapiga risasi na kuwawaua watu tisa mjini Hanau, karibu na Frankfurt. Wahanga wote walikuwa na asili ya uhamiaji. Muuwaji huyo kisha alipatikana akiwa amekufa nyumbani kwake, pamoja na mama yake aliyekuwa na umri wa miaka 72.

Polisi kisha wakakuta barua iliyoelezea maoni ya itikadi kali na video inayojadili nadharia za kiitikadi. Kando na hofu ya mashambulizi ya kulipiza kisasi, usalama umeimarishwa katika misikiti kote Ujerumani kwa sababu inaweza kulengwa katika mashambulizi Zaidi ya itikadi kali.

Uchunguzi wa kisaikolojia kabla ya kumiliki silaha

Wakati huo huo, vyama viwili vya kisiasa Ujerumani vimependekeza uwezakano wa kufanywa vipimo vya lazima vya kisaikolojia kwa wamiliki wa silaha na wanaotuma maombi ya kutaka kumiliki. Helge Lindh, mtalaamu wa masuala ya ndani wa chama cha Social Democratic – SPD ameliambia gazeti la Die Welt kuwa "baada ya shambulizi la Hanau, tunapaswa kutathmini vikali kama tunahitaji kuirekebisha sheria ya umiliki wa silaha.”

Katika toleo la gazeti la Jumamosi la Bild, kiongozi wa chama cha Chjristian Social Union – CSU Horst Seehorfer pia alidai kufanyika vipimo Zaidi vya kisaikolojia katika njia ya "ripoti ya matibabu au uthibitisho” kwa wamiliki wa leseni za silaha. Anasema  lazima ihakikishwe kuwa " kila kitu kiko shwari na kwamba kuyumba kwa akili ya mtu hakuhatarishi usalama wa umma.”

Deutschland Demonstration in Hanau nach Anschlag
Maelfu wakiandamana kulaani mauaji ya HanauPicha: picture-alliance/dpa/A. Arnold

Seehofer amesisitiza kuwa Ujerumani tayari imeimarisha juhudi za kupambana na siasa kali za mrengo wa kulia. Amesema raslimali nyingi zimetolewa kupambana na makundi ya Wanazi-mamboleo, ikiwa ni pamoja na kuwaajiri mamia ya wapelelezi wapya wa serikali na maafisa wa ujasusi wa ndani ya nchi.

Kabla ya shambulizi la Hanau, baraza la mawaziri la Ujerumani liliidhinisha mswada wa kupambana na kauli za chuki na uenezwaji wa itikadi kali kwenye mtandao wa intanet

Maandamano Hanau

Takribani watu 3,000 walifanya maandamano Jumamosi mjini Hanau kupinga chuki na kutouheshimu ubinaadamu. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za polisi. Walibeba mabango yenye ujumbe kama vile "Lazima watu wauawe kwanza ndio mkasirike?” au "Haki za binaadamu badala ya itikadi kali.”

Waandalizi wa maandamano hayo walitarajia washiriki 2,000 katika maandamano hayo kutoka eneo la Freiheitsplatz kumaanisha Eneo la Uhuru – katikati mwa mji huo hadi maeneo mawili ambayo tukio hilo la ufyatuaji risasi lilitokea.