Ujerumani yainyamazisha Ureno | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 17.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Ujerumani yainyamazisha Ureno

Thomas Müller ndiye aliyekuwa shujaa wakati Ujerumani ilipoibamiza Ureno magoli manne kwa bila mjini Salvador. Ureno ilitarajiwa kutoa ushindani mkubwa kwa vijana wa Joachim Löw lakini hilo halikufanyika

Huku ikipambana na kikosi cha Ureno kinachoongozwa na mashambulizi ya Cristiano Ronaldo, Ujerumani ilichukua tahadhari kwa kuwachezesha mabeki wanne. Lakini hatua hiyo hata hivyo haikuonekana kuwa yenye umuhimu wowote kwa mpango wa Löw, kwa sababu vita vilikuwa katika safu ya mashambulizi.

Thomas Müller ambaye alinyakua tuzo ya mfungaji wa magoli mengi katika dimba lililopita la Kombe la Dunia, alifungua ukurasa wa magoli katika dakika ya 11 kupitia mkwaju wa penalty. Hii ni baada ya Joao Pereira kumbwaga chini Mario Götze katika kijisanduku.

Ujerumani iliongeza la pili muda mfupi baada ya nusu saa kupitia beki Mats Hummels aliyeunganisha kichwa safi hadi ndani ya wavu baada ya kona iliyochongwa na Toni Kroos.

Fifa Fußball WM 2014 Deutschland Portugal

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alikuwa miongoni mwa mashabiki wa Ujerumani uwanjani

Maji yalizidi unga kwa upande wa Ureno, wakati Pepe alipoonyeshwa kadi nyekundu kwa kuzozana na Thomas Müller. Kisha muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kukamilika Müller alifunga goli la tatu.

Ujerumani kisha ikapatwa na pigo baada ya Hummels kuondolewa uwanjani kutokana na jeraha la goti. Katika kipindi cha pili, Ureno hawakumsumbua kipa wa Ujerumani Manuel Neuer. Badala yake, Müller alibusu wavu kwa mara ya tatu katika dakika ya 78 na kuipa Ujerumani goli la nne. Kocha wa Ujerumani Joachim Löw amemmiminia sifa mshambuliaji wake bandia Thomas Müller baada ya kuwa mwiba katika safu ya ulinzi ya Ureno. Mueller kawaida hutumika kama mchezaji wa pembeni au kiungo mshambuliaji katika klabu ya Bayern, alidhihirisha kuwa mwindaji hodari.

Loew pia amempongeza beki wake Jerome Boateng aliyekuwa na kibarua cha kumnyamazisha Cristiano Ronaldo. Ghana wanawasubiri Wajerumani mjini Recife mnamo Juni 21 na huku kiwango cha joto kikiendelea kuongezeka, kocha Loew amesema kuwa huenda atafanya mabadiliko katika kikosi chake.

Na kulikuwa na shabiki mmoja katika viti vya mashabiki: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliyeonekana kushangilia kila wakati wavu ulitingisika. Aliwatembelea vijana baada ya mechi ili kuwapongeza na kuwapa motisha.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Mohammed AbdulRahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com