Ujerumani yaikubali jinsia ya tatu | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yaikubali jinsia ya tatu

Mahakama ya juu ya Ujerumani imeamrisha bunge kuitambua "jinsia ya tatu" kutoka siku mtoto anapozaliwa, jambo linaloifanya Ujerumani kuwa nchi ya kwanza ya Ulaya kuwapa watu walio na jinsia mbili uhuru wa kutambulika.

Watu hao sasa watakuwa wanatambulika na jinsia nyengine mbali na mwanamume au mwanamke. Uamuzi huo wa mahakama uliotajwa kama wa kihistoria na shirika linalotetea masuala ya ubaguzi Ujerumani, unaashiria kutikiswa pakubwa kwa sera za jinsia katika nchi hii yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya na haya yanajiri mwezi mmoja baada ya ndoa za jinsia moja kuhalalishwa.

Mahakama hiyo ya kikatiba ilitoa uamuzi wake kutokana na kesi ambapo mlalamikaji aliyetambuliwa kama Vanja na aliyezaliwa mwaka 1989, alikuwa anataka jinsia yake katika usajili wa kuzaliwa ibadilishwe kutoka mwanamke na iwekwe kama mtu aliye na jinsia mbili, ila maafisa walilikataa hilo kwa msingi kwamba sheria inakubali mtoto asajiliwe tu kama mwanamume au mwanamke au iwapo hilo halitofanyika basi, nafasi hiyo katika usajili isijazwe kabisa.

Mwanamume kaaida ana kromosomu X na Y

Mlalamikaji huyo alilalamika kwamba huo ni ukiukaji wa haki zake na katika mapambano ya miaka mitatu kortini, Vanja alitoa ushahidi wa viinitete ulioonesha kwamba ana kromosomu moja ya X ila hana ya pili ambapo kwa kawaida mwanamke anastahili kuwa na kromosomu mbili za X huku mwanamume akiwa na kromosomu moja ya X na moja ya Y.

Italien Gay Pride in Rom (imago/Pacific Press Agency)

Wapenzi wa jinsia moja wakiandamana

Baada ya uamuzi huo, Vanja alikuwa na haya ya kusema.

"Sote tuna utambulisho wa aina fulani, jinsi tunavyojiona au jinsi tunavyojieleza," alisema Vanja. "Na kwa sababu nilikuwa nahisi kwamba hakuna maneno, nafasi wala watu ambao ni vielelezo vyema kwangu, nilikuwa na wakati mgumu wakati nilipokuwa nikikuwa."

Mahakama hiyo iliyoko katika mji wa magharibi wa Ujerumani, Karlsruhe, ilitoa siku ya mwisho ya sheria hiyo kubadilishwa kuwa mwishoni mwa mwaka ujao na imesema imefanya uamuzi wake kutokana na haki za mtu za kimsingi na haki yake ya kulindwa dhidi ya ubaguzi kama ilivyo katika katiba ya nchi hiyo.

Mtu mwenye jinsia mbili anaweza kuwa na viungo viwili vya utambulisho

Mahakama hiyo pia imesema kwa sasa korti na mamlaka za serikali hazistahili kuwalazimisha watu walio na jinsia mbili kutambulika kama wanawake au wanaume, jambo lililoungwa mkono na mtaalam wa masuala hayo Profesa Konstanze Plett.

Leipzig Plakat für eine dritte Option Intersexuelle (picture-alliance/dpa/J. Woitas)

Kwa sasa kuna jinsia ya tatu Ujerumani mbali na mume na mke

"Imethibitishwa na mahakama ya kikatiba nchini kwa mara ya kwanza kwamba, kufanya jinsia ziwe mbili tu, ni jambo linalokiuka haki za wengine," alisema Plett. "Hii sio sawa kabisa kwa kuwa hata ikiwa walio katika hali hiyo ni wachache, haki za wachache zinastahili kuheshimiwa pia, sio lazima liwe suala la makundi ya watu wengi. Na hili limethibitishwa,"aliongeza Profesa huyo.

Kwa kawaida mtu anayetambulika kama aliye na jinsia mbili ni mtu ambaye hawezi kutambulika katika zile jinsia zilizozoeleka za mume na mke, kwa hiyo ni mtu ambaye huenda akawa na viungo ambavyo sio kamili vya kumtambulisha kama mwanamume au mwanamke au anaweza kuwa na viungo vyote kwa pamoja.

Serikali ya Ujerumani imesema itautii uamui huo wa mahakama huku msemaji katika wiara ya masuala ya ndani Johannes Dimroth akisema serikali iko tayari kuitekeleza sheria hiyo.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/APE/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com