1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaUjerumani

Ujerumani yaapa kuvijibu vitisho vya ushuru vya Marekani

19 Januari 2026

Ujerumani inaangazia hatua madhubuti za kujibu kitisho cha Marekani cha kuiwekea ushuru zaidi huku ikionya kwamba vitisho hivyo vya ushuru vya rais Donald Trump havikubaliki na vinazidisha mzozo wa kibiashara.

https://p.dw.com/p/574UA
Ujerumani Berlin 2026 | Lars Klingbeil na Roland Lescure katika mkutano wa masuala ya kifedha nchini Ujerumani na Ufaransa
Lars Klingbeil (kushoto, SPD), Waziri wa Fedha wa Shirikisho, na Roland Lescure, Waziri wa Fedha na Uchumi wa Ufaransa, wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika Wizara ya Fedha ya Shirikisho wakati wa mkutano wa Ufaransa na Ujerumani.Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

"Tumeazimia kujibu kwa hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na ushuru wa kulipiza kisasi. Pia tutaandaa hatua zaidi za sera za kiuchumi ikiwa itatulazimu, pengine mapema Februari,"Msemaji wa serikali ya Ujerumani alisema Jumatatu.

"Kuna makubaliano mapana miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuhusu hili. Ni muhimu kwamba Umoja wa Ulaya sasa uwe na msimamo mmoja kuhusu suala hili," aliongeza.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha wa Ujerumani Lars Klingbeil amesema Ujerumani na Ufaransa zinatafuta namna ya kuyaendeleza makampuni mapya na yanayokua kwa kasi barani Ulaya ili kuyazuia kuhamishia biashara zao nchini Marekani, lakini pia kuunda mazingira bora kwa makampuni mapya.

Bendera za kampuni ya magari ya Ujerumani ya Continental AG, mjini Frankfurt
Bendera za kiwanda cha kutengeneza vipuri vya magari ya Ujerumani ya Continental zikipepea mbele ya jengo la kiwanda hicho huko Frankfurt am Main.Picha: Thomas Lohnes/AFP

Klingel: "Bado kuna safari ndefu"

Klingbel ambaye pia ni makamu wa kansela, alisema hayo katika hafla iliyofanyika Berlin na kuhudhuriwa na mwenzake wa Ufaransa Roland Lescure na kuongeza kuwa makampuni mapya na yenye mafanikio lazima yawe na mtaji wa kutosha na yaweze kukua ndani ya Umoja wa Ulaya soko kubwa zaidi duniani. Hata hivyo, amekiri bado wana safari ndefu kufikia hilo.

Alisema lengo ni kwa makampuni yanayokua na yenye ubunifu kutoka Umoja wa Ulaya kuwa na nguvu kimataifa na kuongeza kuwa ili kufikia hili, mapungufu yaliyopo kwenye ufadhili kwa makampuni kama hayo ni lazima yashughulikiwe.

Ripoti ya kitaalamu iliyokusanywa na waziri wa zamani wa fedha wa Ujerumani Jörg Kukies na gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Ufaransa Christian Noyer ilipendekeza hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kurekebisha mifumo ya pensheni ili kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya uvumbuzi na kuunda muundo sawa wa kisheria wa makampuni kwenya kanda nzima ya Umoja wa Ulaya.