Ujerumani yaamua | Uchaguzi wa Ujerumani 2017 | DW | 24.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani Yaamua

Ujerumani yaamua

Zaidi ya raia milioni 61 wanashiriki katika uchaguzi wa 19 wa bunge la Ujerumani, unaotazamiwa kumrejesha madarakani Kansela Angele Merkel kwa muhula wa nne.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa majira ya saa mbili asubuhi ya leo katika maeneo yote ya uchaguzi nchini Ujerumani, ambapo watu wapatao milioni 61.5 wenye vigezo wanapiga kura katika uchaguzi huu uliosubirwa kwa hamu, na ambamo chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU na chama ndugu cha Christian Social Unioni CSU chenye ngome yake katika jimbo la kusini mwa Ujeurmani la Bavaria kinatabiriwa kushinda kura nyingi zaidi.

Uchunguzi wa maoni ya wapigakura umeuweka muungano wa Merkel wa vyama vya CDU na CSU mbele kwa asilimia 34 hadi 36, dhidi ya asilimia 21 hadi 22 ya chama cha Social Democratic SPD  - uongozi ambao unamaanisha ushindi kwa Merkel ni wa uhakika.

Iwapo matokeo ya uchunguzi huo ni ya kuaminika, uchaguzi wa mwaka huu utashuhudia pia chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative für Deutschland - au Chama Mbadala kwa Ujerumani AfD, kikijishindia viti katika bunge la shirikisho - Bundestag.

Makadiro ya mwanzo ya matokeo ya uchaguzi  huu yanatarajiwa kuanza kutolewa baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura saa 12 jioni kwa saa za Ujerumani, ambazo ni sawa na saa moja jioni  kwa saa za Afrika Mashariki.

Berlin Bundestagswahl Bundespräsident Steinmeier wählt (Reuters/S. Loos)

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeir akipiga kura yake mjini Berlin, Septemba 24, 2017.

Steinmeier: Nendeni mkapige kura

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amewatolea mwito raia leo kwenda kupiga kura, na kusema katika makala yake alioiandika katika gazeti la Bild am Sonntag, kwamba kupiga kura ni wajibu wa kiraia. Kila kura ina umuhimu, alisema Steinmeier na kuogneza kuwa watu wasiopiga wanawaruhusu wengine kuamua mustakabali wa taifa lao.

Kiwango cha ushiriki wa uchaguzi huu kinatarajiwa kuwa juu ya kile cha asilimia 71.5 mwaka 2013. Kwa mujibu wa ofisi ya takwimu ya shirikisho, theluthi moja ya wapigakura wana umri wa zaidi ya miaka 60, huu ukiwa ndiyo umri mkubwa zaidi kwa wapigakura wa Ujerumani. Idadi ya wapigakura wa mara ya kwanza imesalia kwa watu milioni 3.

Kurudi kwa AfD na FDP

Ingawa muhula mwingine kwa Merkel unaonekana ni jambo lililohitimishwa, muungano wake wa CDU/CSU unakabiliwa na uwezekano wa kuhitaji kutafuta mshirika wa kuunda naye serikali, na hivyo matokeo ya vyama kadhaa vidogo yatakuwa muhimu.

Chama cha mrengo mkali wa kulia AfD, kilikuwa na asilimia kati ya 10 na 13 katika uchunguzi wa maoni ya raia, hali ambayo huenda ikakiweka katika nafasi ya tatu nyuma ya vyama vikuu viwili, na kukipa viti zaidi katika Bundestag kuliko chama cha mrengo wa kulia cha Die Linke, au cha watetezi wa Mazingira Die Grüne.

Licha ya mkururu wa matukio yanayozua utata, ikiwemo kiongozi mwenza wa chama hicho Alexander Gauland kusema kwamba kuna baadhi ya masuala ya vita kuu vya pili vya dunia ambayo Ujerumani inapaswa kujivunia, inaonekana misimamo ya AfD ya kupinga uhamiaji na Uislamu imepokelewa vyema na baadhi ya wapigakura.

Berlin Schlange für die Briefwahl zur Bundestagswahl (picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber)

Raia wakitekeleza haki yao ya kupiga kura katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin.

Hatma ya chama kinachoelemea upande wa biashara cha Free Democrats FDP itakuwa muhimu pia. Mwaka 2013 chama hicho alichopendelea Merkel kuunda nacho serikali kilishindwa kuvuka kihunzi cha asilimia tano inayohitajika kuingia bungeni. Lakini safari hii kikimtegemea kiongozi wake machachari Christian Lindner, chama hicho kinatazamia kupata karibu asilimia 9.5 ya kura.

Hata hivyo, hata ushindi huo huenda usitoshe kwa Merkel. Ili kuunda serikali ya wachache, miungano ya Ujerumani inahitaji mamlaka ya asilimia 50 au zaidi, na CDU pamoja na FDP pamoja huenda wasiweze kuvuka kihunzi hicho.

Hii itaviacha vyama vidogo zaidi, kama vile chama cha kijani, na hata chama cha mrengo wa kushoto Die Linke, ingawa kwa uwezekano mdogo sana - kuwa vyama vitakavyoangaziwa katika harakati za kuunda serikali baada ya uchaguzi. Kwa upande wa chama cha AfD, vyamo vyote vikuu vya Ujerumani vimesemawazi kwamba vinakataa kushirikiana na chama hicho kinacholemea siasa kali za kizalendo.

Katika juhudi za mwisho, Merkel, Schulz wahimiza wapigakura

Licha ya tarakimu sawa za utafiti wa maoni ya wapigakura, Merkel na mpinzani wake kutoka SPD, Martin Schulz waliendelea kufanya kampeni kali siku ya Jumamosi, wakitoa miito ya mwisho kwa wapigakura.

Mjini Aachen, karibu na mji wake wa nyumbani, Schulz alifanya jitihada za mwisho kukiokoa chama chake dhidi ya hasara ya kihistoria inachotabiriwa na uchunguzi wa maoni.

TV-Duell Angela Merkel und Martin Schulz (picture alliance/Dpa/dpa)

Wagombea wa vyama vikuu katika uchaguzi wa mwaka huu, kansela Angela Merkel wa CDU, na Martin Schulz wa SPD.

Aliwambia wapigakura kuwa Merkel anataka kuibakiza Ujerumani katika wakati uliopita, kabla ya kukigeukia chama cha AfD na kukitaja kuwa wachimba kaburi ya democrasia, na kuwasihi Wajerumani kukikatilia kuingia bungeni.

Merkel ambaye kampeni yake imejikita kwenye rekodi yake ya kuwa kansela kwa miaka 12 iliopita huku akisisitiza viwango vya chini kabisaa vya ukosefu wa ajira nchini Ujerumani na ukuaji imara wa kiuchumi, alitoa matamshi sawa.

"Wito wangu kwa kila mmoja ni kwamba wapige kura, na wavichaguwe vyama vinavyoheshimu katiba kwa asilimia 100," alisema Merkel, katika matamshi yalioashiria hofu kwamba uitikiaji mdogo wa wapigakura huenda ukakipa mafanikio makubwa chama cha AfD.

Ujerumani inajivunia ushiriki mkubwa wa wapigakura katika uchaguzi ikilinganishwa na mataifa mengine. Mwaka 2013, asilimia 71.5 ya wapigakura walishiriki katika uchaguzi mkuu wa taifa.

Hata hivyo wakati ambapo wengi wakiamini Merkel ataibuka mshindi, juu ya kampeni ya SPD iliyoshindwa kuvutia, haijabanika wazi wangapi watahisi kulaazimika kuelekea vituo vya kupigia kura safari hii.

Mwandishi: Sabine Kinkartz

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Saumu Yusuf.