Ujerumani kufuzu Kombe la Dunia mapema?
Mabingwa hao mara nne wa dunia wamezinduka baada ya kushindwa na hao wapinzani wao wa leo mnamo mwezi Machi mjini Duisburg. Chini ya kocha mpya Hansi Flick, Ujerumani wameshinda mechi zao zote nne za kuwania kufuzu Kombe la Dunia.
"Tunataka kushinda mechi ya kesho. Tunataka kufuzu kwenye Kombe la Dunia haraka iwezekanavyo na mechi ya kesho ni sehemu ya mpango huo," alisema Flick.
Kocha wa zamani wa Ujerumani Joachim Löw aliondoka baada ya mwisho mgumu wa kipindi chake cha ukufunzi kwa kuwa kipigo alichopewa na Macedonia kilifuatia kushindwa 6-0 na Uhispania kabla timu hiyo haijabanduliwa kutoka kwenye mashindano ya Ulaya katika hatua ya timu kumi na sita bora.
Ubelgiji pia inaweza kufuzu Jumatatu
Lakini Flick ambaye ni kocha wa zamani wa Bayern Munich, amewanoa vijana kama Florian Wirtz na Jamal Musiala na mawinga wake Leroy Sane pamoja na Serge Gnabry wameanza kuingilia vyema kimchezo.
Gnabry ni mchezaji wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani.
"Tunataka kushambulia na nguvu mpya. Bila shaka Kombe la Dunia ni lengo kubwa. Bila kufunga mabao ni vigumu kupata ufanisi," alisema Gnabry.
Timu inayoorodheshwa katika nafasi ya kwanza kwenye ramani ya Fifa ya timu bora duniani, Ubelgiji, inaweza kufuzu pia licha ya kutoshiriki mechi hizo kutokana na kushiriki kwake mechi za Nations League ambapo walimaliza katika nafasi ya nne baada ya kufungwa 2-1 na Italia hapo jana.
Ubelgiji inayoongozwa na Roberto Martinez, iko pointi nane mbele ya timu inayoishikilia nafasi ya pili, jamhuri ya Czech pamoja na Wales huku kukiwa kumesalia mechi mbili tu.
Iwapo Wales watapoteza pointi katika mechi yao ambayo hawajaicheza dhidi ya Estonia basi Ubelgiji watakuwa wamejihakikishia kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye hilo kundi lao.
Kwengineko England wanaweza kusogea karibu na kuiabiri ndege ya kuelekea Qatar pale watakapocheza na Hungary katika mechi yao uwanjani Wembley hapo kesho huku wapinzani wao wa karibu katika kundi lao Albania wakiwa wanapambana na Poland mjini Tirana.