Ujangili waendelea kumaliza Tembo Barani Afrika | Masuala ya Jamii | DW | 02.09.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Ujangili waendelea kumaliza Tembo Barani Afrika

Utafiti mkubwa kuwahi kufanywa unaonyesha kuwa Idadi ya tembo barani Afrika inazidi kupungua kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ujangili ambavyoo vimewaangamiza tembo zaidi ya 140,000 kati ya mwaka 2007 na 2014

Tembo aliyekufa baada ya kugongwa na gari

Tembo aliyekufa baada ya kugongwa na gari

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyochapishwa na jarida la Peer J siku ya jumatano utafiti huo umewahusisha tembo wanaopatikana katika ukanda wa savana kutokana na urahisi wa kuonekana ukilinganisha na tembo walioko porini na umeonyesha kuwa idadi ya tembo inazidi kushuka kutokana na kupungua kwa mazingira yao asilia pamoja, lakini sababu kubwa ya kupungua zaidi kwa tembo wa Afrika, ni Ujangili.

Ujangili ambao ulianza kushamiri mwaka 2005 umesababisha vifo vya zaidi ya tembo 30,000 mwaka uliopita

Inakadiriwa kuwa idadi jumla ya tembo walio katika ukanda wa savana katika nchi nchi 18 zilizojumuishwa ni 352,271 ambayo ni asilimia 93 ya tembo wote katika nchi hizo pamoja na kuwa utafiti huo haukuhusisha nchi kama vile Namibia ambako kuna idadi kubwa ya tembo lakini hawakutoa idadi kamili kwa ajili ya utafiti, Sudan Kusini na Jamhuri ya afrika ya kati ambako utafiti huo haukufanyika kutokana na migogoro inayoendelea katika nchi hizo

Serengeti Nationalpark in Tansania

Tembo wakitembea katika Mbuga ya Serengeti nchini Tanzania

Nchi ambazo zimehusishwa katika utafiti huo ni pamoja na Botswana ambayo imechangia maeneo ya tafiti kwa asilimia 37, Zimbabwe imechangia kwa asilimia 23 na Tanzania asilimia 12

Angola, Tanzania na Msumbiji zaongoza kwa vifo vya tembo

Kupatikana kwa miili ya tembo waliokufa ni ishara ya kupungua kwa idadi ya tembo huku ripoti hiyo ikizitaja nchi zinazoongoza kuwa vifo vya wanyama hao ni pamoja na Cameroon, Msumbiji, Angola na Tanzania. wakati nchi ambazo zinaongoza kwa pembe za ndovu ni Msumbiji, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Paschal Shelutete meneja wa mawasiliano wa shirika la hifadhi za Taifa Tanzania TANAPA shirika ambalo ndilo lenye mamlaka ya kusimamia maeneo yaliyotengwa kisheria kama hifadhi za Taifa nchini humo anasema Tanzania kwa upande wake imeanza kufanikiwa kupunguza ujangili kwa mikakati mbalimbali ya kukabiliana nao hii ikiwa inajumuisha kutenga bajeti kubwa kwa ajili ya kuliwezesha shirika hilo kuwa kufanya doria katika maeneo ya hifadhi

Kwa mujibu wa ripoti hiyoya Jumatano, ikiwa ujangili dhidi ya tembo utaendelea utasababisha kutokuwepo kabisa kwa wanyama hao katikia nchi za Mali,Chad na Cameroon wakati ikizitaja nchi za Botswana, Afrika kusini, Zambia na Zimbabwe ambazo zina idadi kubwa ya tembo kuwa hazijaathiriwa sana na ujangili

Mwandishi: Celina Mwakabwale

Mhariri: Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com