1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yachagua bunge jipya kwa mara ya pili mwaka huu

John Juma
10 Novemba 2019

Wahispania wapiga kura kujaribu kumaliza mkwamo wa kisiasa nchini humo. Kulingana na uchunguzi wa maoni, chama cha kisoshalisti cha wafanyakazi PSOE chake Waziri Mkuu Pedro Sanchez, kinatarajiwa kushinda.

https://p.dw.com/p/3SmgD
Spanien Parlamentsneuwahl
Picha: Reuters/S. Perez

Takriban wapiga kura milioni 37 wa Uhispania wapiga kura Jumapili kuchagua bunge jipya. Hii ni mara ya pili kwa uchaguzi mkuu kufanyika nchini humo mwaka huu.

Kulingana na uchunguzi wa maoni, chama cha kisoshalisti cha wafanyakazi PSOE chake Waziri Mkuu Pedro Sanchez, kinatarajiwa kushinda.

Hata hivyo huenda Sanchez asipate wingi wa kutosha bungeni kumwezesha kuunda serikali, hali ambayo inaweza kuendeleza mkwamo ulioko wa kisiasa nchini humo.

Kulingana na takwimu za wizara ya mambo ya ndani, asilimia 37.9 ya raia ndio wamejitokeza kupiga kura. Idadi hiyo imepungua ikilinganishwa na  asilimia 41.5 ya uchaguzi uliopita wa mwezi Aprili.

Kwa miezi kadhaa, Sanchez alijaribu kuunda serikali ya muungano baada ya uchaguzi uliopita wa mwezi Aprili, lakini hakufaulu. Hali iliyomlazimu Mfalme Felipe VI kuitisha uchaguzi mpya.

Hii ni mara ya nne Uhispania inapiga kura ndani ya miaka minne. Kulingana na uchunguzi wa maoni hali hiyo imewachosha wapiga kura wengi, na kusababisha idadi ya wapiga kura wanaojitokeza kupungua ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika uchaguzi wa Aprili.

Kiongozi wa chama cha People's Party Pablo Casada akipiga kura
Kiongozi wa chama cha People's Party Pablo Casada akipiga kuraPicha: Reuters/J. Nazca

Huenda Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Vox, kikaendelea kuimarika na hata kiwe chama cha tatu kwa ukubwa nchini humo. Hayo ni kulingana na chunguzi za maoni, baada ya chama hicho kupata ushindi wa asilimia 10 katika uchaguzi wa Aprili.

Waangalizi wanasema mojawapo ya masuala yatakayoushawishi uchaguzi wa sasa, ni maandamano yanayoendelea katika jimbo la Catalonia, kufuatia kufungwa jela kwa viongozi tisa wa vuguvugu la kupigania uhuru wa jimbo hilo.

Wahafidhina wanamlaumu Sanchez kwa kushindwa kuvunja maandamano na kurejesha sheria na utulivu katika jimbo hilo.

Uchaguzi uliitishwa kwa sababu Sanchez alishindwa kuunda serikali ya muungano pamoja na vyama vingine kama Unidas Podemos au Ciudadanos.

Ikiwa mkwamo utaendelea, basi huenda chama cha kihafidhina cha People's Party (PP) kikajaribu kuunda serikali ya muungano pamoja na vyama vya Ciudadanos pamoja na Vox.

Vyanzo: DPAE, AFPE