1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaondolewa katika mchuano wa Euro 2020

Sudi Mnette
29 Juni 2021

Michezo miwili katika viwanja viwili tofauti ilikuwa na msisimuko wa aina yake, kule Copenhagen, Denmark Uhispania imeichapa Croatia bao 5-3 na Bucharest Ufaransa imefungishwa virago na Uswisi kwa kupigwa mabao 5-4.

https://p.dw.com/p/3viwW
EURO 2020 | Frankreich vs Schweiz | Kylian Mbappe
Picha: Justin Setterfield/REUTERS

Michezo miwili katika viwanja viwili tofauti ilikuwa na msisimuko wa aina yake, kule Copenhagen, Denmark Uhispania imeichapa Croatia bao 5-3 na Bucharest Ufaransa imefungishwa virago na Uswisi katika mchuano huo wa Euro 2020 kwa kupigwa mabao 5-4 ya mikwaju ya penati ikiwa ni baada ya kutoka suluhu wa mabo 3-3 katika duru ya 16 ya mchuano huo kabambe.

Katika mchezo wa awali, wachezaji wa Uhispania  Alvaro Morata na Mikel Oyarzabal waliwainua washabiki wao uwanjani baada ya kuingiza nyavuni mabao mawili katika muda wa nyongeza na hivyo kuifanya timu yao kuibuka na ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Croatia.

Uhispania imekata tiketi ya kuingia katika hatua ya robo fainali.

Uhispania ambayo kwa ushindi huu wa sasa  inakata tiketi ya moja kwa moja ya kuingia katika hatua ya robo fainali, haijakuwa ikifanya vizuri katika michuano mingi ya kimataifa tangu iisambaratishe Italia katika mchuano kama huu wa euro 2012.

Na katika mchezo ambao ulikuwa na msisimuko zaidi kati ya Ufaransa na Uswisi, hatma imekuwa Ufaransa kuwekwa pembeni mwa mchuano huo, baada ya mchezaji wake nyota Kylian Mbabe kukosa mkwaju muhimu wa penati. Kwa hivyo Uswisi imeweza kuondosha klabu bingwa ya kombe la dunia kwa mnyukano wa mikwaju ya penati au kwa  maneno ya kisoka, magoli ya matuta.

Baada ya mchuano mkali ambao uliiacha miamba hiyo ya soka kwa mabao 3-3, ililazimika waingie katika hatua ya penati ili kuweza kumpata mshindi wa kuendelea katika hatua ya robo fainali.

Yann Sommer, golikipa mtetezi wa Uswisi kutoka katika mapumziko ya uzazi.

EURO 2020 | Frankreich vs Schweiz
Golikipa wa Uswisi Yann Sommer Picha: Justin Setterfield/REUTERS

Golikipa wa Uswisi, Yann Sommer, ambae alijiondoa kwa muda katika timu hiyo katika hatua ya makundi, kwa lengo la kuungana na mkewe baada ya kujifungua mtoto wa kike, alifanya maajabu ya kucheza vyema katika mwaju wa penati wa 10, baada mingine tisa kama huo kuingia wavuni.

Kwa hivyo Uswisi sasa itarajiewe kufuana na Uhispania katika hatua ya robo fainali huko St. Petersburg  katika kipute kitakachopigwa Ijumaa, kwa siku hiyo hiyo Ubelgiji itafuana na Italia mjini Minuch. Na michezo mingine katika hatua hii ya sasa ya mtoano itafanyika jioni ya leo (29.06.2021) ambapo Ujerumani itakaribishwa na England mjini London na kule Glasgow, Sweden itafuana na Ukraine.

Chanzo: AP