1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Ujerumani: Wagombea wahitimisha kampeni

Angela Mdungu
25 Septemba 2021

Wagombea wawili wenye uwezekano mkubwa zaidi wa kushika nafasi ya kansela ajaye wa Ujerumani, Olaf Scholz na Armin Laschet, wanakamilisha kampeni zao za mwisho leo, kabla ya uchaguzi utakaofanyika kesho Jumapili

https://p.dw.com/p/40qR4
Deutschland I Wahlplakate in Frankfurt am Main
Picha: Arne Dedert/dpa/picture alliance

Utafiti wa maoni ya raia unaonesha tofauti ndogo kati ya wagombea hao huku Scholz wa chama kinachofuata nadharia ya mrengo wa wastani wa kushoto SPD akiwa mbele ya Laschet wa CDU kwa asilimia tatu pekee.

Kansela anayemaliza muda wake Angela Merkel, ambaye ameliongoza taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi barani Ulaya kwa karibu miaka 16, anamuunga mkono mwanachama mwenzake wa chama cha kihafidhina cha CDU Armin Laschet, katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni huko Aachen alikozaliwa mgombea huyo. 

Symbolbild Abschied der Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani anayemaliza muda wake Angela MerkelPicha: Swen Pförtner/dpa/picture alliance

Scholz wa chama cha SPD yuko kwenye kampeni za mwisho katika jimbo la Brandenburg, lililo karibu na mji mkuu. Mgombea wa tatu kutoka chama cha kijani, Annalena Baerbock, amehitimisha kampeni zake akiwa kwenye nafasi ya tatu katika utafiti huo wa maoni, huku akipewa nafasi ndogo ya kuwa kansela. Hata hivyo chama chake kinatarajiwa kuimarisha zaidi nafasi yake kwenye uchaguzi huu ikilinganishwa na ule wa mwaka 2017, na huenda kikahusika katika kuunda serikali ya pamoja.

Muungano wa vyama vitatu unatarajiwa

Waangalizi wengi wa uchaguzi wanatarajia matokeo yatasababisha kuwa na serikali inayohusisha vyama vitatu, lakini bado haijawa wazi ni vyama vipi vitakavyokuwemo. Ikiwa kambi ya Laschet inayoundwa na vyama ndugu CDU/CSU kitaongoza, serikali ya muungano itakayoundwa inatarajiwa kuwa ya mrengo wa kati na kulia.

Kama chama cha SPD kikishinda, basi Ujerumani inaweza ikabadilika kidogo ama kuchukua kabisa mwelekeo mpya wa siasa za mrengo wa kushoto kutegemeana na ni nani atakayechaguliwa na Scholz kuwa mshirika wake. Uwezekano mwingine ni kuwa Ujerumani inaweza kuendelea na serikali ya muungano wake wa sasa unaoundwa na vyama vya SPD na CDU/CSU