1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Kenya: Wanawake, vijana uongozini

Sandner, Philipp8 Machi 2013

Huku Kenya ikiendelea kuzihesabu kura, wale waliochaguliwa katika nyadhifa mbali mbali baadhi yao wakiwemo wabunge, magavana na maseneta wanaendelea kusherekea ushindi wao, miongoni mwao wakiwa vijana na wanawake.

https://p.dw.com/p/17tQ4
People discuss the presidential elections results in the western town of Kisumu, 350km (218 miles) from the capital Nairobi, March 7, 2013. The running mate of Kenya's presidential candidate Raila Odinga called for the vote count to be halted on Thursday and cast doubt on the fairness of a process that is still incomplete three days after the poll, remarks that could inflame a largely peaceful election. REUTERS/Thomas Mukoya (KENYA - Tags: POLITICS ELECTIONS)
Kenia nach den Wahlen 2013Picha: Reuters

Kijana mmoja wa Baringo ana kila sababu ya kutabasamu baada ya kujinyakulia ushindi katika wadhifa wa mwakilishi wa kata katika sehemu hiyo. Kibiwott Munge ambaye ana miaka 19 aliwapiku wanasiasa wenye umri wa juu na tajriba ya miaka mingi kwa kujizolea kura zaidi ya 3,333.

Huyu ndiye kiongozi wa pili aliyewahi kuchaguliwa akiwa na umri mdogo zaidi baada ya Proscovia Angelot aliyeshinda kiti cha ubunge katika jimbo la Usuk huko Uganda mwaka jana na kuwa kiongozi mchanga zaidi wa Kiafrika kushinda ubunge.

Huko Kajiado, mwanamke wa Kimaasai ameshinda uchaguzi wa ubunge na kuwa mwanamke wa kwanza kabisa kuwahi kuwania na kushinda nafasi ya uongozi katika jamii hiyo iliyo na itikadi kali dhidi ya uongozi wa wanawake.

Peris Pesi Tobiko sasa ndiye mbunge mteule wa Kajiado baada ya kukabiliana na wimbi kali la upinzani kutoka kwa viongozi wa jamii hiyo.

Bi Tobiko huenda ni mgeni katika masuala ya siasa lakini ni jina la kutajika katika nyadhifa za uongozi katika mashirika mengi hasa ya kijamii na taasisi kadhaa za kiserikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.

Mvulana akiwa amevaa kofia na kukaa kwenye pikipiki.
Mvulana akiwa amevaa kofia na kukaa kwenye pikipiki.Picha: Reuters

Peris Pesi Tobiko amekuwa mstari wa mbele ndani ya jamii hiyo ya Wamaasai katika kuwashajiisha na kuwaelimisha wanawake kuhusu haki zao za kimsingi.

Na si Peris Tobiko pekee ambaye anawashangaza wengi kwa kunyakua kiti katika uchaguzi huu, bali kuna Profesa Hellen Sambili ambaye amenyakua kiti cha ubunge cha Mogotio kwa tiketi ya chama cha KANU ambacho katika miaka ya hivi karibuni kimekuwa hakina wafuasi na kuonekana kufutika kabisa katika ramani ya siasa za Kenya na mahala pake kuchukuliwa na chama cha URP kinachohusiswa na William Ruto.

Katika eneo hilo hilo la Bonde la Ufa, Alexander Kimutai ambaye ni mtoto wa mbunge wa Emgwen anayeondoka madarakani, ameshinda kiti cha ubunge wa sehemu hiyo, huku baba yake, Henry Kosgey, akishindwa kupata kiti cha useneta alichokuwa akiwania kwa tiketi ya chama cha ODM. Alexander mwenye umri wa miaka 29 aliwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha URP.

Naye Mike Mbuvi anayejulikana kwa jina la mtaani kama Sonko, ingawa ana miaka 46, ndiye amekuwa seneta wa kwanza kabisa aliyepigiwa kura kutokana na ujana wake. Sonko alikiwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha TNA kilicho katika muungano wa Jubilee unaoongozwa na Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta.

Mwandishi: James Muhando
Mhariri: Yusuf Saumu