1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi: Mzozo wa DRC ni "mauaji ya kimbari"

24 Septemba 2025

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuutambua mzozo wa mashariki mwa nchi yake kuwa ni "mauaji ya kimbari yanayoendeshwa kimya kimya".

https://p.dw.com/p/50zlh
New York 2025 | Felix Tshisekedi akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la UN
Rais wa DRC Felix Tshisekedi akiuhutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, MarekaniPicha: Eduardo Munoz/REUTERS

Akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo jana, Rais Tshisekedi alisema zipo dalili zote zinazoashiria vitendo vya maangamizi yaliyopangwa akisisitiza kuwa huo sio tu mzozo wa kawaida bali ni mauaji ya kimbari yanayofanyika kimyakimya na ambayo yamekuwa yakiathiri watu wa Kongo kwa zaidi ya miaka 30.

Tshisekedi  ametoa wito wa kuanzishwa kwa tume huru ya kimataifa itakayokuwa na jukumu la kufanya uchunguzi ili kusaidia "kutokomeza mfumo wa kutowajibishwa" ambao amesema umechochea janga hili kwa miongo kadhaa, huku akisisitiza pia umuhimu wa uwepo wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya wahusika wa vitendo vya "uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinaadamu na mauaji ya kimbari" yaliyofanywa katika eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri mkubwa wa madini.

Tshisekedi ailaumu Rwanda kuendeleza mzozo 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Tshisekedi aliitupia lawama Rwanda kwa kuendelea kuwaunga mkono waasi wa M23 na kutoonyesha nia ya kutekeleza  makubaliano ya amani yaliyosainiwa mjini Washington:

New York 2025 | Felix Tshisekedi akiwasili katika Mkutano wa Baraza Kuu la UN
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi akiwasili katika Mkutano wa Baraza Kuu la UN mjini New York , MarekaniPicha: Leonardo Munoz/AFP

"Hatua ya kusitisha mapigano haijafanikiwa kwa kuwa Rwanda inafahamu kuwa hilo likiwezekana, itakuwa ndio mwisho wa harakati zake Kongo. Vita hivi si vya kisiasa bali vya kiuchumi ambavyo vinatukabili ili wahusika waendelee kupora rasilimali zetu. Na hiyo ndio sababu pekee na ya kweli inayofanya Rwanda kutumia nguvu zote hizo ili kuyumbisha usalama mashariki mwa Kongo."

Uchunguzi wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa ulibaini uwezekano wa pande zote zinazohusika katika mzozo huo kutenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Ghasia zimeongezeka tangu mwaka 2021 baada ya kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda kuibuka tena na kufanikiwa mapema mwaka huu kuchukua udhibiti wa miji mikuu ya  Goma na Bukavu . Kulingana na Umoja wa Mataifa, mapigano yaliyozuka tangu Januari, 2025 yamesababisha vifo vya maelfu ya watu huku malaki ya wengine wakilazimika kuyahama makazi yao.

Ufaransa kuandaa mkutano kuhusu DRC

New York 2025 | Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akihutubia mkutano wa UN
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: Eduardo Munoz/REUTERS

Rais Emmanuel Macron ametangaza kuwa Ufaransa itaandaa mwezi ujao wa Oktoba mjini  Paris  mkutano wa dharura utakaojadili hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa nchini DRC huku akisisitiza kuwa katika eneo la Maziwa Makuu, mamlaka na mipaka ya Kongo ni lazima viheshimiwe, na akielezea umuhimu wa kurejesha matumaini kwa wakazi wa Kivu na watu wote ambao wamelazimika kulikimbia eneo hilo. 

Hata hivyo, waangalizi wanahofia mashambulizi ya M23  dhidi ya mji wa Uvira wenye wakazi 500,000 katika jimbo la Kivu Kusini ambao bado uko chini ya udhibiti wa jeshi la Kongo na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya Kinshasa. Kuvamiwa kwa mji wa Uvira uliokaribu mno na nchi jirani ya Burundi kunaweza kusababisha msuguano kati ya Kigali na Bujumbura na hivo kupelekea mzozo huo kuwa wa kikanda.

// AFP