1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump haendi COP30, lakini Marekani inashiriki mkutano huo

Kübler Martin
11 Novemba 2025

Licha ya kwamba utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umeupa kisogo mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira wa COP30 unaofanyika Belem, lakini baadhi ya viongozi wa ngazi ya chini wa kitaifa na majimbo wanashiriki.

https://p.dw.com/p/53Rn2
USA Washington D.C. 2025 | Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Jacquelyn Martin/AP Photo/dpa/picture alliance

Jumuiya ya kimataifa kwa kiasi kikubwa ilitarajia kwamba utawala wa sasa wa Marekani hautohudhuria mkutano huo wa COP30. Rais Trump ameiondoa Marekani kutoka Mkataba wa Paris kwa mara ya pili, kupunguza ufadhili wa nishati mbadala, kupigia upatu miradi ya nishati ya visukuku na kuwaeleza viongozi wa ulimwengu katika hadhara ya Mkuatano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Septemba kwamba mabadiliko ya tabia nchi "ni ulaghai mkubwa zaidi kuwahi kufanywa dunianni."

Lakini wajumbe kutoka jimbo la Washington, pamoja na Magavana, Mameya na wawakilishi wengine kutoka kwenye majimbo na miji ya Marekani, wamedhamiria kurekebisha hilo. Kwa pamoja, wanawakilisha karibu theluthi mbili ya wakaazi wa Marekani na kuzalisha karibu robo tatu ya pato la kiuchumi la nchi hiyo.

Jay Inslee, gavana wa zamani wa Democratic huko Washington aliyesafiri kutoka Seattle hadi Rio nchini Brazil alipozungumza na DW alisema kwamba ilikuwa ni muhimu kwake na wenzake kushiriki mazungumzo hayo.

Mkutano wa kilele wa Tabianchi, COP27 waanza Misri

Aliongeza kwamba "Marekani haijajiondoa Mkataba wa Paris, ila ni sehemu moja tu ya nchi hiyo ambayo ni serikali ya shirikisho." Inslee ni mwanachama mwanzilishi wa Muungano wa Mazingira wa Marekani, muungano wa magavana wa vyama viwili vya kisiasa ambao unajumuisha majimbo 23 na eneo moja.

Je, Ushuru wa Trump utazorotesha COP?

Wakati timu ya Trump ikitarajiwa kutohudhuria mkutano wa mjini Belem, baadhi ya wadadisi wana wasiwasi kwamba kiongozi huyo anaweza kutibua mazungumzo hayo kutokea mbali. Shinikizo kutoka Washington lilizuia juhudi za kutoza ushuru wa kwanza wa usafirishaji kaboni duniani mwezi uliopita na kuvuruga mkataba ulioongozwa na Umoja wa Mataifa wa kukomesha uchafuzi wa plastiki mwezi Agosti.

"Utawala wa Trump unatoa shinikizo kwenye mazungumzo hayo kupitia sera yake ya ushuru," alisema Maha Rafi Atal, profesa msaidizi katika kitengo cha uchumi wa siasa kwenye Chuo Kikuu cha Glasgow. Aliiambia DW kwa njia ya barua pepe, jinsi rais huyo alivyojaribu kushinikiza Umoja wa Ulaya kutoyatoza ushuru wa forodha wa kaboni makampuni ya Marekani kwa makubaliano ya kulegeza ushuru.

Brazil Belém 2025 | Wanaharakati wa mazingira wakiandamana wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP30
Wanaharakati wa mazingira wakiandamana wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP30Picha: Igor Mota/ZUMA/picture alliance

"Ishara iliyotumwa kwa nchi duniani kote ni kwamba Marekani inaweza kuziadhibu kwa masharti ya biashara nchi ambazo huchukua hatua kali za mazingira," aliongeza Atal.

Lakini mwenyekiti mwenza wa shirika la 'Marekani ni Yote' AIAI Gina McCarthy anabainisha kwamba "viongozi wa ndani na wafanyabiashara wa Marekani wanahimiza nishati safi na wako tayari kushirikiana na wadau wa kimataifa ili kuimarisha Mkataba wa Paris katika kuayakabili mabadilko ya tabia nchi."

Juhudi za ndani zaongezeka

Zaidi ya Viongozi 100 wa ngazi ya chini wa kitaifa wa Muungano wa mazingira wa Marekani, wakiwemo Mameya na wale wanaowakilisha maafisa wa serikali na majiji pamoja na jamii za asili zenye utawala wa ndani, wafanyabiashara, shule na taasisi zingine wanashiriki katika mazungumzo ya mjini Belem huko Amazon, ambayo yalianza Novemba 10 yakitarajiwa kukamilika Novemba 21.

Ingawa maamuzi mengi katika COP yanaathiri jinsi mataifa yanavyokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika ngazi ya shirikisho, viongozi wa eneo hilo wanaamini Marekani, nchi ya pili kwa uchafuzi wa mazingira duniani baada ya China, bado inaweza kufikia malengo ya Mkataba wa Paris wa 2015 na kufikia uzalishaji wa hewa chafu usiozidi sifuri kufikia katikati mwa karne.