Trump azishambulia Korea Kaskazini, Iran na Venezuela | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

MAREKANI

Trump azishambulia Korea Kaskazini, Iran na Venezuela

Rais Donald Trump amewahimiza wanachama wa Umoja wa Mataifa kuiwekea shinikizo Korea Kaskazini kuachana na silaha zake za kinyuklia akisema suala hilo ni  moja ya changamoto kubwa duniani.

Trump amesema dunia inakabiliwa na kitisho kikubwa kutoka kwa mataifa korofi pamoja na ugaidi na wanamgambo waliyo na misimamo mikali. Rais huyo wa Marekani ameapa kusambaratisha itikadi kali.

Trump ametaka nchi zitangulize maslahi yao kwanza kama anavyotanguliza yeye  maslahi ya Marekani. Amesema kwa muda wote atakaokuwa madarakani atatetea maslahi ya Marekani kuliko kitu kingine chochote.

Trump amesema mkataba kati ya mataifa makubwa na Iran ulikuwa fedheha na kuongeza ya kwamba raia wa Iran wanahitaji mabadiliko huku akiitaja serikali ya Iran kama taifa lenye ukorofi lililoishiwa kiuchumi ambalo mauzo yake makuu ya nje ni vurugu.

Pia kiongozi huyo wa Marekani amezikosoa vikali tawala za kijamaa za Cuba na Venezuela, huku akimtaja kwa jina kiongozi wa Venezuela nicolas Maduro na kumkosoa kwa kukandamiza demokrasia.

Rais huyo wa Marekani pia amempongeza  Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa kutamka kwamba Umoja huo unahitaji mageuzi.

Nordkorea testet Antrieb für Satellitenrakete Kim Jung Un (Reuters/KCNA)

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jung Un, amekataa kabisa kuachana na mipango yake ya silaha kali.

Awali Guterres alisema dunia inakabiliwa na changamoto chungu nzima ikiwemo ukosefu wa usalama, kutokuwa na usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa migogoro na mabadiliko ya tabia nchi. 

Akiwahutubia wajumbe wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, amesema uchumi wa dunia unatangamana zaidi lakini hisia zetu za jamii ya kimataifa huenda zikawa zinatengana.

Antonio Guterres ameongeza kuwa jamii zinazidi kugawanyika huku hali ya kisiasa ikiwekwa mahala pamoja, na kuaminiana nchi kwa nchi kukipungua kukisababishwa na wale wanaogawana na kuchochea vurugu huku akiongeza kuwa sasa hivi dunia imekuwa ya vipande na inahitaji kuwa dunia ya amani. 

Akiuzungumzia mgogoro wa Korea Kaskazini Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema mamilioni ya watu wanaishi kwa hofu kufuatia majaribio ya makombora yanayofanywa na Korea Kaskazini.

Hata hivyo China na Urusi zimeonya kuwa matamshi ya  Marekani juu ya matumizi ya nguvu za kijeshi huenda yakasababisha janga la kidunia  na badala yake zinasisitiza juu ya mazungumzo ya kidiplomasia. 

Mwandishi Amina Abubakar/AP/AFP/Reuters 
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com