Trump azindua kampeni ya 2020 kwa malalamiko | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.06.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump azindua kampeni ya 2020 kwa malalamiko

Rais Donald Trump amezindua kampeni ya kuwania muhula wa pili katika mkutano uliogubikwa na malalamiko na matamshi ya visasi kuliko kubainisha ajenda yake kwa mhula wa pili.

Jumanne usiku katika mji wa Orlando jimboni Florida, Trump alilalamika kwamba amekuwa chini ya mashambulizi tangu siku ya kwanza ya urais wake kutoka kwa kile alichokitaja kuwa "vyombo vya habari za uzushi" na uwindwaji haramu wa kisiasa, ambavyo vimejaribu kumtuliza yeye na wafuasi wake.

"Kwa miaka miwili na nusu iliyopita, tumekuwa chini ya mzingiro. Na kwa ripoti ya Mueller tulishinda na sasa wanataka mwendelezo. Wanataka kuliendeleza. Tulifanye tena. Haikwenda vizuri. Tufanye tena. Wanataka mwendelezo," alisema rais huyo.

Trump startet offiziell US-Wahlkampf für 2020 (Reuters/C. Barria)

Trump na mke wake Melania wakiwasili jukwani kuzindua rasmi kampeni ya kuchaguliwa kwa muhula wa pili mjini Orlando, Florida, Juni 18,2019.

Trump alichora taswira ya kutia wasiwasi ya nini kinaweza kutokea ikiwa atashindwa katika uchaguzi huo wa 2020, akiuambia umati wa wafuasi wake kwamba "Wademocrat wanataka kuwaharibu, na wanataka kuiharibu nchi yetu kama tunavyoijua."

Lugha hiyo ya kufa na kupona na unyooshaji vidole vilibainisha wazi kwamba kampeni ya Trump ya uchaguzi wa 2020 itafanana kwa sehemu kubwa na ile ya 2016.

'Saa na nusu ya uongo, upotoshaji na upuuzi'

Mgombea wa chama Democratic Seneta Bernie Sanders alisema baada ya kuanza kwa mkutano huo wa Trump kwamba kiongozi huyo yuko mbali sana na mahitaji ya watu wa kawaida, na kumtaja kuwa mtu anaepaswa kushindwa.

"Nimepata uzoefu usiopendeza kumsikiliza na hata kumuona Donald Trump. Wow. Na bila shaka hilo lilikuwa jambo. Saa moja na nusu ya hotuba za uongo, upotoshaji na upuuzi mtupu. Huo ni uzoefu wa aina yake," alisema Sanders baada ya hotuba ya Trump.

Florida, Bernie Sanders (picture-alliance)

Seneta Bernie Sanders, mgombea wa tiketi ya chama cha Democratic kuwania urais ameikosoa hotuba ya Trump kuwa ilijaa uongo, upotoshaji na upuuzi.

Seneta huyo wa jimbo la Vermont ndiye alikuwa mgombea pekee wa chama cha Democrat miongoni mwa wagombea zaidi ya 20 wanaotafuta tiketi ya kuogmbea nafasi hiyo kumjibu Trump mara moja baada ya hotuba yake.

Timu ya kampeni ya makamu wa zamani wa rais Joe Biden ilitoa taarifa saa moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa Trump ambapo meneja wake wa kampeni Kate Bedinfield, alisema nchi inakabiliwa na chaguo la ama kumfanya Trump kuwa punguani au kumuacha aubadilishe kimsingi na milele mwenendo wa taifa hilo.

Vyanzo: Mashirika

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com