Trump awahimiza Warepublican kufanikisha mswada wa afya | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Trump awahimiza Warepublican kufanikisha mswada wa afya

Baadhi ya maseneta tayari wameelezea kutoridhishwa kwao na mswada wa afya uliopitishwa wiki iliyopita wakihofia uwezekano wa mfumo huo kuwa wa gharama za juu kwa wakongwe na wale ambao tayari wanaugua.

Mjadala tata wa kugeuza mfumo wa afya Marekani unaelekea katika bunge la seneti huku Mrepublican mwenye msimamo wa kadri Susan Collins akisema baraza la seneti halitapokea mswada uliopitishwa bali baraza hilo litaanza upya. Hayo yakijiri rais wa Marekani Donald Trump, amewahimiza Warepublican kutowaangusha wamarekani katika mjadala huo tata utakaofanyika wiki au miezi michache ijayo.

Baadhi ya maseneta tayari wameelezea kutoridhishwa kwao na mswada wa afya uliopitishwa wiki iliyopita wakihofia uwezekano wa mfumo huo kuwa wa gharama za juu kwa wakongwe na wale ambao tayari wanaugua maradhi ya kudumu kando na kupunguzwa kwa fedha za kuwahudumia kiafya.

Seneta Susan Collins kutoka jimbo la Maine ambaye ni mwanachama wa Republican mwenye msimamo wa kadri amesisitiza kuwa bunge la seneti halitajadili mswada uliopitishwa bali wataandika mswada mpya na anaamini watatumia muda wao vyema kuandaa mswada mzuri.

Spika Paul Ryan (katikati)

Spika Paul Ryan (katikati)

Collins pia alilalamika kuwa bunge liliharakisha mswada huo kabla ya ofisi inayoshughulikia bajeti kutathmini faida na hasara zake.

Mick Mulvaney ambaye ni mkurugenzi wa bajeti katika utawala wa Trump, naye amesema, mswada utakaowasilishwa kwa rais utatofautiana na uliopitishwa na bunge. Hali ambayo italazimu mabunge yote mawili kushirikiana na kupatana kuhusu mswada utakaoungwa mkono na mabunge yote.

Trump aitia doa mfumo wa afya "Obamacare"

Katika juhudi za kupigia debe mswada huo wa kufanyia mageuzi bima ya afya iliyoanzishwa na mtangulizi wake rais mstaafu Barack Obama, Rais Donald Trump mnamo Jumapili kupitia ukurasa wake wa Twitter aliwahimiza maseneta wa Republican kutoawaangusha Wamarekani. "Warepublican hawatawaangusha Wamarekani. Matozo kwa bima ya afya ya Obama na ada nyinginezo zake ni juu sana. Ilikuwa uwongo na sasa imekufa" Ndivyo Trump alivyoandika.

Kwa Upande wake rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama aliyatetea mafanikio ya bima hiyo akisema "ninatumai maseneta wa sasa watakumbuka kuwa haihitajiki ujasiri mwingi kuwasaidia wale ambao tayari wanao uwezo, waliotulia na wenye ushawishi. Lakini inahitajika ujasiri kuwatetea wanyonge, wagonjwa na wasiojiweza."

Waandamanaji wakipinga mageuzi ya bima ya afya

Waandamanaji wakipinga mageuzi ya bima ya afya

Mashirika makubwa na makundi yanayohusika na masuala ya afya kikiwemo chama cha wahudumu wa afya Marekani kimepinga mswada huo wa afya. Wademocrat pia wanakataa kushiriki katika hatua yoyote ya kuondoa bima iliyoko iliyoanzishwa na Obama. Kadhalika baadhi ya maseneta wa Republican wanapinga kupunguzwa kwa matumizi ya fedha kwa huduma za afya kwa masikini na walemavu.

Gavana John Kasich wa Ohio aliuliza nini kitakachowakuta watu wenye matatizo ya akili, waathiriwa wa dawa za kulevya na wanaougua maradhi hatari yasiyotibika ikiwa mageuzi yanayopendekezwa yatatimizwa? Watakuwa wanaishi katika hatari kuu. Alibashiri.

Spika wa bunge la Marekani, Paul Ryan ameonekana kubadili msimamo wake wa awali huku akisema "tunafikiri tunapaswa kuwasaidia zaidi wakongwe na wale ambao wanaugua maradhi ya kudumu". Alisema akiongeza kuwa bunge la seneti litakamilisha kazi iliyosalia.

Mwandishi: John JUma/EAPE

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com