Trump avurumuka na kuondoka mkutanoni kwa hasira
Donald Trump alivurumuka na kutoka katika mkutano na viongozi wa mabaraza ya bunge la Marekani " nilisema kwaheri," aliandika katika ukurasa wa Twitter muda mfupi baada ya mkutano huo, wakati juhudi za kumaliza kufungwa kwa sehemu shughuli za serikali, ziliingia katika mparaganyiko mkubwa. Mamia kwa maelfu ya wafanmyakazi wa serikali wanakabiliwa sasa na kukosa mishahara hadi kesho Ijumaa.
Wakati atakaposimama kwa muda leo mjini McAllen , Texas , Trump atafanya ziara katika kituo cha mpakani cha doria kwa ajili ya mazungumzo kuhusiana na uhamiaji na usalama wa mpakani, na kupata maelezo kuhusu usalama wa mpaka. Lakini Trump ameelezea shaka shaka yake kwamba kujitokeza kwake pamoja na matamshi hayatabadilisha mawazo ya mtu yeyote, wakati akitafuta kupata dola bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta ambao umekuwa ni ahadi yake kuu tangu alipokuwa akifanya kampeni ya urais.
Mazungumzo hayo yalizusha uvumi zaidi juu ya iwapo Trump atatangaza dharura ya kitaifa na kujaribu kuidhinisha ujenzi wa ukuta huo binafsi iwapo baraza la Congress halitaidhinisha fedha anazotaka.
Mkutano ulioparaganyika
Katika siku ya 19 ya kufungwa kwa sehemu ya shughuli za serikali kulikosababishwa na kutokubaliana kuhusiana na ujenzi wa ukuta huo, mkutano mfupi kati ya Trump, kiongozi wa maseneta kutoka chama cha Democratic Chuck Schumer na spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi pamoja na viongozi wengine ulimalizika katika mparaganyiko na hakuna ishara ya kupatikana suluhisho.
"Alimuuliza spika Pelosi, "Unakubaliana na ukura wangu?" Alisema hapana. na alisimama na kusema " kwahiyo hakuna cha kujadili. " na aliondoka. "Na tukliona hasira na hamaki kwasababu hakuweza kupata kile anachotaka na aliondoka tu kwenye mkutano.
Mkutano huo uliofanyika katika Ikulu ya White House ulimalizika baada tu ya dakika 14. Wademokrati walisema walimuomba Trump kufungua serikali lakini aliwaambia iwapo atafanya hivyo watampa fedha kwa ajili ya ujenzi wa ukuta.
Warepublikan wamesema Trump aliuliza swali la moja kwa moja kwa spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi , kwamba iwapo atafungua serikali , anaweza kutoa fedha za kugharamia ujenzi wa ukuta ? Alisema hapana. Trump alikwenda katika jengo la bunge mapema jana Jumatano, akitaka kuwatuliza wabunge wa chama chake wasio na msimamo thabiti. Na aliondoka ajisifu kuwa chama chake kiko pamoja kabisa.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Caro Robi