Trump apata ushindi wa kishindo | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.03.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Trump apata ushindi wa kishindo

Bilionea Donald Trump ameshinda tena majimbo matatu kwa mpigo kwenye kura za mchujo kuwania ugombea urais wa Marekani, huku Hillary Clinton na Bernie Sanders wakigawana ushindi wa Missisipi na Michigan.

Donald Trump wa Republican akizungumza na wafuasi wake mjini Michigan.

Donald Trump wa Republican akizungumza na wafuasi wake mjini Michigan.

Ulikuwa ni usiku wa raha kwa Trump, lakini wenye mchanganyiko wa kicheko na kilio kwa Clinton na Seneta Sanders.

Bilionea Trump alimtangulia kwa mbali mshindani wake wa karibu, Ted Cruz, kwenye majimbo mawili muhimu ya Missisipi na Michigan.

Bilionea huyo mwenye misimamo mikali dhidi ya wahamiaji na wageni, anaripotiwa pia kushinda kwenye jimbo la Hawaii.

Kwa upande wake, Clinton alimuangusha Sanders kwenye jimbo linalokaliwa na Wamarekani wengi wenye asili ya Afrika, Missisipi, lakini ni Sanders aliyeibuka mshindi wa jimbo jengine muhimu la Michigan.

Trump ambaye hata hivyo, aliangushwa na Cruz kwenye jimbo la Idaho, aliwaambia wafuasi wake mjini Michigan kwamba sasa ana uhakika wa kuwa rais wa Marekani.

"Tupo mbele kwa kiasi cha asilimia 50 au zaidi. Hapo unazungumzia mamilioni ya watu. Naamini kabisa kuwa hii ni habari kubwa kabisa kwenye siasa, na ninatarajia Warepublican wataipokea. Tuna Democrat wanakuja, tuna wagombea huru wanakuja, lakini hawana idadi hiyo, na pengine kamwe hawatakuwa nayo," alisema Trump.

Waziri wa zamani wa mambo ya nje, Clinton, alilichukuwa kwa urahisi jimbo la ghuba ya kaskazini la Missisipi, ambalo kimsingi lina wafuasi wengi wa Democrat.

Tayari mke huyo wa rais wa 42 wa Marekani, ameshajikingia zaidi ya nusu ya kura wa wajumbe 2,382 zinazohitajika kuteuliwa kupeperusha bendera ya kuwania kiti hicho, akiwekeza zaidi kampeni zake kwenye uwezo wa Wamarekani kujiamini katika kuleta mabadiliko, mfano wa ilivyokuwa kampeni ya Rais Barack Obama.

Hillary Clinton awa Democrat akizungumza na wafuasi wake mjini Missisipi.

Hillary Clinton awa Democrat akizungumza na wafuasi wake mjini Missisipi.

"Usimruhusu mtu kukwambia kuwa hatuwezi tena kufanikiwa Marekani. Tunaweza, tunafanikiwa na tutafanikiwa. Lakini ili hilo liwe, hatuwezi kujenga kwenye kuta kongwe au kurejesha majira ya saa nyuma. Tunapaswa kujenga juu ya kile kinachoifanya Marekani kuwa taifa kubwa, nishati, matumaini, uwazi na ubunifu wetu," aliwaambia wafuasi wake.

Sanders bado aonesha dhamira

Lakini licha ya kuwa hisabati za kura zinamuweka Clinton mahala pazuri zaidi, mpinzani wake Sanders ameibuka kuwa mwanasiasa mwenye dhamira ya dhati ya kusonga mbele.

Katika jimbo la Michigan, mzee huyo wa miaka 74 ambaye ana uzoefu wa harakati za kisiasa kwa zaidi ya miaka 50, amemuangusha Clinton kwa asilimia 2, akiwavutia sana vijana kwa kampeni yake ya mapinduzi ya umma, usawa wa kiuchumi na mapambano dhidi ya kile anachokiita "mfumo wa kifisadi wa kisiasa"

"Watu wa Marekani wanasema kuwa wamechoka na mfumo wa kifisadi wa kampeni na ufadhili wa matajiri wakubwa, Wall Street na tabaka la mabilionea. Wamechoka na uchumi unaoibiwa ambapo watu wa Michigan, Illinois, Ohio, wafanya kazi kwa masaa mengi kwa mshahara wa kiwango cha chini, wakiwa na wasiwasi na mustakabali wa watoto wao," alisema mjini Michigan.

Wachambuzi wanasema hata kama Sanders hatafanikiwa kuitwaa tiketi ya Democrat kuwania urais, kama ambavyo amewahi kuikosa huko nyuma, athari yake kwenye siasa za sasa za Marekani ni kubwa mno kuweza kudharaulika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Caro Robi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com