Trump amtimua mkurugenzi wa mawasiliano | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.08.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Marekani

Trump amtimua mkurugenzi wa mawasiliano

Rais wa Marekani Donald Trump amemfukuza kazi mkurugenzi wake wa mawasiliano baada ya kuutumikia wadhfa huo kwa muda wa siku 11 tu. Anthony Scaramucci anakuwa mkurugenzi wa tatu kuondolewa madarakani.

Rais Donald Trump amemwengua mkurugenzi wake wa mawasiliano Anthony Scaramucci katika kipindi cha chini ya wiki mbili tangu kumteua. Bwana Scaramucci aliingia matatani kwa sababu ya kutumia lugha isiyostahili dhidi ya wafanyakazi wenzanke.

Taarifa juu ya kutimuliwa Scaramucci ilitolewa muda mfupi tu baada ya rais wa Marekani Donald Trump kumuapisha mkuu mpya wa utumishi kwenye ikulu bwana John Kelly aliyemmwagia sifa nyingi. Trump alisema Jenerali Kelly atafanya kazi nzuri itakayoonekana, na hana shaka juu ya hilo kwani aliyoyatimiza alipokuwa mkurugenzi wa usalama wa ndani yamevuka sifa zote.  Trump amsema kazi aliyofanya Jenerali Kelly imeleta mafanikio makubwa.

John F. Kelly (Picture-Alliance/AP Photo/S. Walsh)

John Kelly mkuu mpya wa utumishi katika Ikulu ya Marekani

Jenerali mstaafu John Kelly muda mfupi baada ya kuapishwa kwake alimweleza mkurugenzi wa mawasiliano Anthony Scaramacci kuwa kibarua chake kimefika mwisho. Kwa mujibu wa gazeti la New York Times Anthony Scaramucci amefukuzwa kutokana na maombi ya mkuu huyo mpya wa utumishi John Kelly.  katika tamko lake ikulu ya Marekani imesema bwana Scaramucci ameona kwamba ni bora kumpa mkuu mpya fursa na uwezo wa kujijengea timu yake.  Msemaji wa ikulu Sarah Huckabee Sanders amewaambia waandishi wa habari kwamba hakuna mipango yoyote ya kumpa bwana Scaramucci wadhifa mwingine katika serikali ya Donald Trump.

Scaramucci ni mkurugenzi wa mawasiliano wa tatu kuondolewa ikulu, baada ya Michael Dubke na Sean Spicer.  Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema kutimuliwa kwa mkurugenzi huyo wa tatu kunathibitisha jinsi utawala wa Trump unavyokabiliwa na changamoto kubwa.  Je kuteuliwa mkuu mpya wa utumishi John Kelly kutarudisha utulivu katika utawala wa Trump?

Kwa mujibu wa msemaji wa ikulu Sarah Sanders mkuu huyo mpya John Kelly ambaye ni jenerali mstaafu atakuwa na mamlaka kamili ya kufanya kazi zake kwa kadiri atakavyo ona kuwa ni sahihi.  Msemaji huyo wa ikulu ameeleza kwamba watumishi wote wa ikulu ikiwa pamoja na binti yake Trump, Ivanka, Mumewe Jared Kushner na mkuu wa mikakati Steve Bernnon watawajibika kwa mkuu huyo mpya. Bibi Sanders amesema kwamba John Kelly atajenga muundo mpya, ataleta nidhamu na nguvu mpya katika ikulu.

Baadae Rais Donald Trump aliitisha mkutano na baraza lake zima la mawaziri akiwemo mwanasheria mkuu Jeff Sessions ambaye hivi karibuni alitolewa maneno hadharani na rais Trump.  Hata hivyo msemaji wa ikulu Sarah Sanders alikanusha uvumi kwamba mabadiliko mengine yananukia katika ikulu ya rais Donald Trump.

Mwandishi:Zainab Aziz/APE/dw.com/p/2hT7t

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com