1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UtandawaziKimataifa

Trump: Marekani haitatumia nguvu kuipata Greenland

Lilian Mtono rtre,dpae,afpe,ape
21 Januari 2026

Rais Donald Trump ametumia jukwaa la WEF Davos kufufua azma ya Marekani kuipata Greenland, lakini amesisitiza hatatumia nguvu. Lakini viongozi wa NATO wameonya kuwa mkakati wake unaweza kuisambaratisha jumuiya hiyo.

https://p.dw.com/p/57C9j
Uswisi Davos 2026 | Rais wa Marekani Donald Trump akiwa jukwaani katika Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos
Rais wa Marekani Donald Trump akihudhuria mkutano wa 56 wa kila mwaka wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos, Uswisi, Januari 21, 2026.Picha: Denis Balibouse/REUTERS

Rais wa Marekani Donald Trump amelitumia Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos kusisitiza azma yake ya Marekani kudhibiti kisiwa cha Greenland, akisisitiza kuwa hatatumia nguvu kufanikisha lengo hilo.

Akizungumza mbele ya viongozi wa dunia, Trump alisema kuwa ni Marekani pekee yenye uwezo wa kulilinda na kulihakikishia usalama eneo hilo la Denmark, akitoa wito wa kufanyika "mazungumzo ya haraka” kuhusu uwezekano wa kukinunua Greenland.

"Watu walidhani nitatumia nguvu, lakini sihitaji kufanya hivyo. Situmii na sitatumia nguvu,” alisema Trump katika hotuba yake Davos.

Kauli hizo zilitolewa wakati Trump akirejea Davos baada ya miaka sita, hatua iliyofanya uwepo wake kugubika ajenda nzima ya mkutano wa siku tano wa WEF.

Hotuba hiyo, iliyotarajiwa kujikita zaidi kwenye uchumi wa Marekani, iligeuka kuwa jukwaa la mashambulizi ya kisiasa dhidi ya washirika wa Ulaya.

Trump aliwakosoa vikali washirika wa Marekani barani Ulaya, akiwatuhumu kwa "kukosa shukrani, kukosa uaminifu na kufanya makosa ya sera” katika masuala ya mazingira, nishati ya upepo, uhamiaji na jiografia ya kisiasa.

Uswisi, Davos 2026 | Rais wa Marekani Donald Trump akiwa na Mkuu wa WEF Børge Brende wakati wa mkutano wa mwaka
Rais wa Marekani Donald Trump na Mkuu wa WEF Børge Brende wakizungumza wakati wa Mkutano wa 56 wa WEF mjini Davos, Uswisi, Januari 21, 2026Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Greenland, NATO na hofu ya Ulaya

Vitisho na kauli za Trump kuhusu Greenland zimezidisha wasiwasi barani Ulaya na kuendelea kudhoofisha uhusiano wa kuvuka Atlantiki. Viongozi wa NATO wameonya kuwa mkakati huo unaweza kuyumbisha muungano huo wa kijeshi.

Trump aliipuuza hoja kwamba azma yake ni tishio kwa NATO, akieleza kuwa suala la Greenland ni "ombi dogo” kuhusu "kipande cha barafu,” huku akimtaja Denmark kama "asiye na shukrani.”

"Hakuna taifa wala kundi la mataifa linaloweza kulinda Greenland isipokuwa Marekani,” alisisitiza.

Katika hotuba yake iliyodumu zaidi ya saa moja, Trump pia alikosea mara kadhaa kwa kuiita Greenland kama Iceland, hali iliyozua gumzo miongoni mwa washiriki.

Licha ya msimamo wake mkali, viongozi wa Denmark na Greenland wamesema wako tayari kupanua ushirikiano wa kijeshi na kiusalama na Marekani bila kubadili umiliki wa eneo hilo lenye wakazi wapatao 57,000.

Uswisi, Davos 2026 | Tim Cook, Jensen Huang na Christine Lagarde katika Jukwaa la Uchumi Duniani kabla ya hotuba ya Donald Trump
Mkurugenzi Mtendaji wa Apple Tim Cook, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa NVIDIA Jensen Huang, na Rais wa Benki Kuu ya Ulaya (ECB) Christine Lagarde, kabla ya hotuba ya Trump.Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Trump ajinasibu kwa uchumi wa Marekani

Mbali na Greenland, Trump alitumia jukwaa la Davos kujinasibu kuhusu utendaji wa uchumi wa Marekani, akidai kuwa "muujiza wa kiuchumi” unaendelea kutokea.

"Marekani ni injini ya uchumi wa dunia. Marekani inapoimarika, ninyi mnafuata,” aliwaambia viongozi wa dunia.

Alisisitiza kuwa sera zake zimefanikiwa kupunguza mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi, huku akidai Ulaya "haiendi katika mwelekeo sahihi.”

Trump pia aliilaumu serikali ya awali ya mrengo wa kati-kushoto kwa kushuka kwa uzalishaji wa umeme nchini Ujerumani, akisema uzalishaji umepungua kwa zaidi ya asilimia 22 tangu 2017.

Umoja wa Ulaya waanisha kujibu vikali vitisho vya Trump

Onyo kwa Umoja wa Mataifa na msimamo wa NATO

Katika hatua nyingine, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ujerumani na Rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock alisema Umoja wa Mataifa unakabiliwa na "mashambulizi ya moja kwa moja,” huku kukiwa na hofu kwamba Trump anaweza kuanzisha chombo pinzani cha kimataifa.

Alisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unabaki kuwa jukwaa pekee ambapo mataifa yote 193 yana uwakilishi sawa, bila kujali nguvu au utajiri wao.

Kwa upande wa NATO, Katibu Mkuu Mark Rutte aliwataka wanachama wa muungano huo kutoruhusu mvutano wa Greenland kuathiri mshikamano wao katika kuisaidia Ukraine.

Hata hivyo, Rutte alikiri kuwa Trump ana hoja inapokuja suala la umuhimu wa kimkakati wa eneo la Arctic, akisisitiza kuwa usalama wa eneo hilo ni wajibu wa pamoja.

Uswisi, Davos | Washiriki wa Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) katika Kituo cha Mikutano cha Davos (Davos Congress Centre)
Washiriki wa World Economic Forum wakiwa wamepanga foleni kwenye ngazi zinazoelekea ukumbi mkuu wa mikutano katika Davos Congress Centre.Picha: Ashutosh Pandey/DW

Davos chini ya kivuli cha Trump

Mamia ya wajumbe walikusanyika katika kumbi na maeneo ya wazi ya Davos kusikiliza au kufuatilia hotuba ya Trump kupitia skrini na simu zao. Baada ya zaidi ya saa moja, baadhi yao walionekana kupoteza hamasa na kurejea mazungumzo ya pembeni.

Kurejea kwa Trump Davos kumesisitiza mabadiliko ya mpangilio wa dunia, kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa, na maswali mazito kuhusu mustakabali wa usalama wa Arctic, NATO na uhusiano wa Marekani na washirika wake wa jadi.

WEF Davos 2026 imegeuka kuwa zaidi ya kongamano la uchumi — imekuwa kioo cha dunia inayozidi kugawanyika.