Trump achelewesha amri mpya kuhusu wahamiaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Trump achelewesha amri mpya kuhusu wahamiaji

Ikulu ya Marekani imechelewesha kutangaza amri mpya za rais za kuchukua nafasi ya marufuku ya awali ya kuwazuia raia wa mataifa saba ya Kiislamu kuingia nchini humo.

Tangazo hilo limetolewa muda mfupi kabla ya Marekani kubatilisha sheria inayowaruhusu wanafunzi kutumia vyoo kulingana na jinsia wanazofuata.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sean Spicer, jana aliwaambia waandishi habari kwamba amri hizo mpya ambazo zilikuwa zitangazwe wiki hii, sasa zitatangazwa wiki ijayo. Spicer amesema suala lililopo hivi sasa ni kuona amri gani ambazo zitasainiwa na rais na iwapo watakuwa na suala rasmi la kulitangaza, watafanya hivyo.

Amri za awali zilizotangazwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, zilikuwa zinawazuia wananchi wa Iraq, Syria, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen kuingia nchini Marekani kwa siku 90. Pia aliwazuia wakimbizi wote kutoingia nchini humo kwa siku 120 na wakimbizi wa Syria walizuiwa kwa muda usiojulikana. Baadhi ya wachambuzi wanatarajia utaratibu mpya hautokuwa na tofauti na ule uliotangazwa awali.

Trump amesema amri mpya zitashughulikia masuala ya kisheria yaliyozushwa na majimbo Washington, San Francisco na maeneo mengine kuhusu agizo la mwanzo lililotolewa Januari 27. Amri hizo zilizokosolewa na makampuni maarufu ya Marekani na washirika wa nchi hiyo pamoja na kuzua tafrani kwenye viwanja vya ndege, ziliwafanya Wamarekani wagawanyike. Mahakama za Marekani zilizuia amri hizo kwa muda, hatua iliyokosolewa na Marekani.

Trump afuta agizo jingine la Obama

Hayo yanajiri wakati ambapo Rais Trump pia ameifuta haki ya sheria inayolinda wanafunzi wa mapenzi ya jinsia moja ambayo ilikuwa inawaruhusu wanafunzi hao kutumia vyoo na mabafu kulingana na jinsia wanazofuata. Agizo hilo lilitolewa na mtangulizi wa Trump, Barack Obama Mei 2016, ambapo aliagiza shule za umma kuwakubali wanafunzi wanaoegemea jinsia tofauti na zile walizozaliwa nazo.

USA Unisex-Toilette in New York (picture alliance / AP Photo)

Ishara zinazoelekeza choo na bafu la watu wasiotaka kuonyesha jinsia zao

Barua zinazoelezea mabadiliko hayo yaliyofanywa na Trump, zimetumwa katika shule za umma nchini Marekani na zinafafanua kuwa agizo la Obama lilikuwa linasababisha hali ya sintofahamu na lilikuwa likizusha utata, hali iliyosababisha kuwa gumu kutekelezeka.

Wakati huo huo, Mkuu wa Haki za Binaadamu katika wizara ya mambo ya ndani nchini Mexico, Roberto Campa amesema mpango wa Marekani uwarejesha raia wasio wa Mexico nchini humo ni uhasama na haukubaliki. Viongozi wa Mexico wameelezea hasira yao kuhusu sera biashara na uhamiaji za Rais Trump, kabla ya mkutano wa leo kati yao na maafisa waandamizi wa Marekani, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Rex Tillerson na Waziri wa Usalama wa Ndani, John Kelly.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico, Luis Videgaray amesema hakuna namna yoyote kwa Mexico kuzikubali sheria mpya za Trump, miongoni mwao zikiwa za kuwarejesha raia wasio wa Mexico nchini humo.

''Nataka kuweka wazi kwamba msiwe na wasiwasi wowote. Mexico na serikali ya Mexico haitosita kwenda katika mashirika ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, haki za binaadamu na uhuru kwa ajili ya wananchi wa Mexico wanaoishi nje ya nchi,'' amesema Videgaray.

Videgaray, amesema Mexico haitokubali masharti ambayo nchi moja inataka kuyaweka kwa ajili ya nchi nyingine. Viongozi hao wa Marekani pia wanatarajiwa kukutana na Rais wa Mecixo, Enrique Pena Nieto na maafisa waandamizi wa usalama, uchumi na wanadiplomasia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, AFP
Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com