Tanzania yasitisha safari za kuelekea India | Matukio ya Afrika | DW | 05.05.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Tanzania yasitisha safari za kuelekea India

Serikali ya Tanzania imesitisha safari zake za ndege kwenda nchini India ikiwa ni hatua mojawapo ya kukabiliana na kuenea kwa mlipuko mpya wa maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua hiyo imechukuliwa siku moja baada ya serikali kutoa mwogozo mpya unaowalenga wasafiri wanaoingia nchini humo kutoka mataifa ambayo yanashuhudia maambukizi ya juu ya virusi hivyo, wakitakiwa kujiweka karantini kwa siku 14. 

Taarifa ya wizara ya afya inasema safari zote za ndege kutoka India zimepigwa marufuku kwa muda usiojulikana hadi hapo itakapoarifiwa tena baadaye na marufuku hiyo inaanza kazi mara moja.

Awali shirika la ndege la taifa, ATCL lilitangaza kusitisha safari zake mjini Mumbai, India, lakini hatua ya serikali kupiga marufuku ndege zote kutoka India kuingia nchini inaashiria hatua yake ya kujaribu kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 kutoka katika eneo hilo.

Tanzania haiwezi kujitenga na ulimwengu katika kushughulikia janga la corona

Mataifa ya India na Brazil yamekuwa yakiripoti ongezeko kubwa maambukizi mapya ya virusi vya corona na kuna ripoti kuwa baadhi ya maofisa wa serikali walioko nchini India wameathiriwa na janga hilo.

Serikali ya Tanzania katika siku za hivi karibuni imekuwa ikichukua mwelekeo mpya wa kukabiliana na janga hilo ikiwamo kuunda jopo maalumu la wataalamu wanaofuatilia mwenendo tatizo hilo na imeanza kuwaraia wananchi kuchukua tahadhari.

Tazama vidio 01:32

Janga la Covid-19 laitikisa India

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyeko ziarani nchini Kenya, amesema Tanzania haiiwezi kujitenga na ulimwengu katika kushughulikia kadhia hiyo na amehimiza wataalamu wa afya wa Tanzania na Kenya mataifa ambayo awali yalikuwa yakichukua mkondo tofauti dhidi ya janga hilo kutafuta njia bora ya kuwa na kauli moja.

Kama hatua ya kuongeza udhibiti dhidi ya janga hilo, wizara ya afya imetoa mwongozo mwingine kwa wageni wanaoingia nchini ambao sasa watapaswa kufanyiwa vipimo vya ziada hata kama wanazo nakala vya vyeti kuonyesha hawana maambukizi.

Wananchi wanastahili kuzingatia kanuni za afya badala ya mijadala ya kujitia hofu

Watapaswa kufanyiwa tena kipimo kidogo kitakachowagharimu dola za Marekani 25. Awali wizara hiyo ilitoa masharti ambayo yanawataka wasafiri wote wanaotoka katika mataifa yenye kiwango kikubwa cha maambukizi kujiweka karantini kwa siku 14 wakijigharimia wenyewe.

Indien Corona-Pandemie | Situation in Ghaziabad

India imelemewa na wimbi la maambukizi ya virusi vya corona

Mjadala kuhusu uwezekano wa kurejea upya kwa maambukizi ya virusi vya corona umeanza kujitokeza katika maeneo mengi ya nchini hasa kutokana na uhusiano wa karibu baina ya raia wa Tanzania wenye asili ya India ambao wamekuwa wakirejea nchini.

Hata hivyo, Waziri wa afya, Dorothy Gwajima amewataka wananchi kutojiingiza katika mijadala yenye kuzua hofu na badala yake kuendelea kuzingatia kanuni za kiafya.

Hadi sasa hakuna taarifa zozote rasmi kuhusu kuwepo kwa wagonjwa wapya wa COVID-19 nchini Tanzania.