Tanzania ilipata hasara ya dola milioni 50, intaneti kuzimwa
27 Februari 2026
Hayo yameelezwa katika ripoti mpya ya tathmini ya ufwatiliaji wa 'Utawala wa Mtandao' wa Tanzania kwa mwaka 2025, iliyoangazia uadilifu na uhuru wa Sekta ya Habari nchini wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Serikali ya Tanzaniaimeshauriwa kurejesha majukwaa ya kidijitali bila masharti sambamba na kuharakisha utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa Akili Mnemba unaozingatia haki za binadamu.
Hayo yamebainishwa katika ripoti mpya iliyozinduliwa jana na Taasisi ya Masuala ya Dijitali ya Tech and Media Convergency ya nchini Tanzania iliyofanya tathmini ya mfululizo wa 'Utawala wa Mtandao wa Intaneti nchini Tanzania wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Haki za Binadamu pia zilikiukwa 'gizani'
Akizungumzia yale yaliyobainishwa zaidi katika ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Media Convergency, Asha Abdinala amesema, sambamba na hasara kubwa iliyotokana na kuzimwa wa mtandao wa intaneti kadhalika haki za kiraia zilivunjwa.
Soma pia: Familia Tanzania bado zatafuta miili baada ya vurugu za uchaguzi
“Tumelenga kutoa hii ripoti kiwa kama kielelezo cha kuonyesha hali ipoje na inaendeleaje, tumetoa pia maoni kwa upande wa serikali kwa mfano kuangalia baadhi ya sheria zinazotawala mtandao wa intaneti na sheria zinazotawala vyombo vya habari,” amesema Abdinala.
Kadhalika ripoti hiyo imebaini kuwa, katika kipindi hicho, ukatili wa kijinsia mtandaoni uliongezeka kwani Takwimu kutoka shirika la wanawake katika sheria Afrika -WiLDAF, zilirekodi jumla ya maoni hasi 3,644 yaliyomlenga mwanasiasa mwanamke maarufu.
Ukatili wa kijinsia waongezeka mitandaoni Tanzania
Mkurugenzi wa chama cha wanahabari wanawake Tanzania, TAMWA- Dk Rose Reuben aliyeshiriki uzinduzi wa ripoti hiyo, amezungumzia matokeo ya ripoti hiyo kuhusu udhalilishaji wa wanawake wanasiasa mtandaoni.
“Na katika ripoti hii tumeona kwamba ukatili wa kijinsia mtandao umeongezeka sana na hili ni eneo ambalo TAMWA imekuwa ikigusia sana kwa sababu tumeona kwamba, ukatili wa kijinsia umehama majumbani na sasa umehamia mitandaoni jambo ambalo limesababisha wanawake kuzikimbia na kuzikosa fursa zinazoletwa na mitandao ya kijamii,” Reuben amesema.
Ripoti hiyo imeshauri serikali ya Tanzania kuhakikisha kuna uwajibikaji; kufuta au kurekebisha kwa kiasi kikubwa kanuni za vikwazo vya maudhui ya mtandao na kurekebisha masharti yasiyoeleweka katika mtandao wa Vyombo vya Habari.
Kimsingi ripoti hiyo imebaini kuwa katika kipindi cha mwaka 2025 kulikuwa na asilimia 52 ya matukio yaliyochagiza ukandamizaji wa uhuru wa kidijitali na uhuru wa kujieleza mtandaoni.
Hata hivyo ripoti hiyo imebaini kuwepo kwa asilimia 28 .7 ya jitihada za dhati za serikali na wadau wa serikali katika kuimarisha utawala wa intaneti na mifumo ya kidijitali Tanzania.