Zipi athari za kufungwa kwa mitandao Tanzania?
7 Novemba 2025
Baada ya ukimya uliosababishwa na maandamano na machafuko yaliyodumu kwa siku nne, shughuli za kijamii na kiuchumi zimerejea nchini Tanzania. Mamlaka nchini humo pia zimerejesha huduma ya intaneti iliyokuwa imefungwa wakati wa vurugu za mandamano yaliyotikisa mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Songwe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na DW, waandishi habari na watengeneza maudhui mitandaoni wamesema walipata wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yao kutokana na kuzimwa kwa internet.
Wamesema kuwa kuzimwa kwa mtandao huo wa internet kumesababisha athari kubwa na nyingi ikiwemo kupoteza mapato, kutokana na watengenezaji maudhui mitandaoni kutengemea mapato yanayotokana na habari ama maudhui wayachapishayo mitandaoni.
Fredrick Bundala ambaye ni mkurugenzi wa chombo cha habari cha mtandaoni cha Simulizi na Sauti (SNS), anasema asilimia mia moja ya maudhui wayatengenezayo yanategemea intaneti na kwamba kwa kipindi chote ambacho internet ilifungwa hawakuweza kufanya kazi ya kuuhabarisha umma na hivyo kupoteza pia mapato.
“Kwa kipindi cha siku sita ambazo hakukuwa na internet, maana yake ni kwamba hatukuweza chochote katika kipindi hicho, kwahiyo athari imekuwa kubwa ambayo impact yake itaendelea kuwepo kwasababu kuna wafanyakazi inabidi uwalipe mshahara kwa huu mwezi kuanzia tarehe 29 mpaka mwanzoni hapo wa tarehe mbili mwezi huu wa 11, maana yake hatukuweza kuzalisha chochote. Kwahiyo athari imekuwa kubwa sana.”
Kwa upande wake Juventus Mugendani ambaye pia ni mwandishi wa habari na mtengezaji wa maudhui mtandaoni jijini Dodoma Tanzania anasema changamoto kubwa ilikuwa ni kushindwa kupandisha maaudhui kutokana na kufungwa kwa intaneti:
“Kwahiyo niseme tu kwamba tulishwa kupandisha maudhui lakini pia changamoto nyingine ilikuwa ni huduma za kifedha, kwasababu tunafahamu kuwa mtandao ndio kila kitu. Niseme tu kwamba hiyo ni moja ya kitu kilichokuwa kinashindikana kwahiyo huwezi kufanya muamala wa aina yoyote, lakini pia naweza nikasema kwamba shughuli zote ambazo zilikuwa zinahusiana na masuala ya mtandao ilikuwa ni ngumu lakini kwasababu ilikuwa ni nchi nzima basi tuliweza kulipokea kwasababu ni sababu ambazo ni kwa ajili ya usalama wa taifa.”
Kufungwa kwa huduma ya internet kulisababishwa na maandamano ambayo yalianza siku ya uchaguzi, yakisababisha vifo na majeruhi kadhaa pamoja na uharibifu mkubwa wa mali hasa za umma na binafsi za watu wanaohusishwa na utawala.