Tamasha kupinga wanazi lafanyika Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.09.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Tamasha kupinga wanazi lafanyika Ujerumani

Kiasi cha watu 65,000 walifurika katika tamasha la kupinga matukio ya kibaguzi Jumatatu usiku ikiwa ni pamoja na vitendo vya chuki dhidi ya wageni,

Bendi kadhaa maarufu nchini Ujerumani zilitumbuiza  katika mji huo wa mashariki mwa Ujerumani kuwasilisha ujumbe kupinga vitendo vya kibaguzi kufuatia tukio la shambulizi la kisu dhidi ya mwanamme mmoja wa Ujerumani mnamo August 26. Wanaume wawili mmoja raia wa Iraq na mwingine wa Syria tayari wametiwa mbaroni wakihusishwa na tukio hilo.

Ni polisi 1,800 tu waliosambazwa  katika mji wa Chemnitz hapo Jumamosi mnamo wakati   jimbo  la Saxony likishutumiwa  kuruhusu polisi wachache katika maandamano Jumatatu.

Zaidi ya bendi tatu maarufu nchini Ujerumani ziliwatumbuiza waandamanaji hao wengi wao wakiwa ni vijana jana usiku wanaounga mkono uwepo wa wahamiaji nchini Ujerumani chini ya kauli mbiu isemeayo "SISI TUKO WENGI ZAIDI".

Maafisa wa mji wa Chemnitz walisema idadi ya watu waliohudhuria tamasha hilo jana usiku ni 65,000. Waandaaji wa tamasha hilo la jana walisema walitaka kuonesha kuwa hakuna nafasi katika mji wa Chemnitz kwa watu wenye mtizamo wa Kinazi.

Tamasha hilo liliungwa mkono na watu wengi

Deutschland, Chemnitz: Konzert gegen Rassismus (picture-alliance/dpa/S. Willnow)

Baadhi ya walioshiriki tamasha mjini Chemnitz kupinga wanazi

Hata hivyo tamasha hilo ilibidi lihamishiwe sehemu nyingine badala ya sehemu ya awali baada ya idadi ya watu wahudhuriaji kuongezeka. 

Mmoja wa wanamuziki waliotumbuza kwenye tamasha hilo wa bendi ya Krraftklub alisikika akisema wao si watu wasiojitambua, huku akisisitiza kuwa wakati mwingine kuna haja ya kuonesha kuwa wahamiaji hawako peke yao.

Tamasha hilo lilianza kwa kukaa kimya kwa dakika moja kama ishara ya kumkumbuka mtu aliyeuawa katika shambulizi la kisu huku polisi wakisema hakukuwa na vurugu wakati wa saa za awali za tamasha hilo.

Maafisa wa mji wa Chemnitz waliwazuia wafuasi wa kundi la Pegida  katika mji wa Chemnitz wasiandamane kupinga tamasha hilo.

Hayo yanajiri mnamo wakati watuhumiwa wawili wanaoshikiliwa hadi sasa wakihusishwa na shambulizi la kisu wakihojiwa hapo jana ingawa msemaji wa upande wa mashitaka hakutoa maelezo zaidi. 

Taarifa ambazo bado hazijathibitishwa zinazodai kwamba mwanaume huyo aliyeuawa alikuwa akimlinda mwanamke mmoja wa Kijerumani dhidi ya washambuliaji ndizo zilizoibua ghadhabu katika baadhi ya vitongoji vya mji huo.

Mwandishi: Isaac Gamba/dpae

Mhariri: Mohammed Khelef    

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com