Taasisi ya kuchunguza benki za Ulaya kuundwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Taasisi ya kuchunguza benki za Ulaya kuundwa

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuziweka benki zote za bara la Ulaya chini ya taasisi moja ya uchunguzi mwaka ujao, lakini wakashindwa kutangaza tarehe kamili ya kuanza mpango huo.

European Union leaders pose for a family photo at a EU summit in Brussels October 18, 2012. EU leaders will try to bridge deep differences over plans for a banking union at a summit on Thursday but no substantial decisions are expected, reviving concerns about complacency in tackling the three-year-old debt crisis. REUTERS/Christian Hartmann (BELGIUM - Tags: POLITICS BUSINESS)

Brüssel EU-Gipfel Gruppenbild

Hata hivyo muafaka wa taasisi hiyo kuundwa mwaka ujao, uliokubaliwa katika mkutano huo wa kilele uliodumu saa 11 mjini Brussels, utaziruhusu benki zinazoyumba kupokea fedha moja kwa moja kutoka kwa hazina za uokozi barani Ulaya.

Uamuzi huo ulifikiwa wakati kukiwa na mazingira tulivu ya masoko barani Ulaya hapo jana, lakini pia wakati kukishuhudiwa ghasia zilizozuka upya nchini Ugiriki. Huko ndiko mgogoro huu uliodumu miaka mitatu ulianzia, baada ya mwanamme mmoja kufariki wakati wa mgomo na maandamano ya kupinga hatua za kubana matumizi.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akihutubia mjini Brussels

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akihutubia mjini Brussels

Viongozi 27 wa Umoja wa Ulaya waliweka wenyewe malengo ya kukubaliana kuhusu mfumo wa kisheria ifikapo Januari mosi mwaka wa 2013. Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo ilisema kazi ya kuanzisha taasisi hiyo itafanywa katika mwaka huo wa 2013. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliutaja mpango huo kuwa maono makubwa, wakati Rais wa Ufaransa Francois Hollande akishinikiza utekelezaji wa haraka.

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso amesema mkuu wa Benki ya Umoja wa Ulaya, Mario Draghi aliwaambia viongozi hao kuwa kutekelezwa mpango huo kunaweza kuchukua chini ya mwaka mmoja lakini kwa hakika zaidi ya mwezi mmoja au miwili.

Rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy alikiri kuwa hawezi kupeana tarehe kamili, lakini akasema mawaziri wa fedha watakutana tarehe 12 Novemba mwaka huu, na kulijadili suala hilo. Wazo la msingi la kuundwa taasisi hiyo ni kuwa, katika siku za usoni, benki zinazoyumba katika mataifa yanayokabiliwa na madeni na ambayo yanahatarisha mfumo wa kiuchumi barani Ulaya zinaweza kupewa mitaji moja kwa moja kutoka kwa hazina za uokozi za Umoja wa Ulaya.

Maandamano ya kupinga hatua za kufunga mkaja Ugiriki

Maandamano ya kupinga hatua za kufunga mkaja Ugiriki

Viongozi pia walisifu hatua nzuri zilizopigwa nchini Ugiriki katika kutekeleza mageuzi yanayolenga kuuimarisha uchumi, baada ya kundi la wakopeshaji wake kusema kuwa linataraji kufikia mkataba katika siku chache zijazo wa kurejelea ufadhili wake. Serikali ya kihafidhina ya Ugiriki inafanya mazungumzo na kundi la wahisani wake kuhusu mfuko wa uokozi unaohitajika kuwezesha malipo ya mkopo wa euro bilioni 31, ambayo yamekuwa yakisubiri tangu mwezi Juni.

Polisi wa kupambana na ghasia nchini Ugiriki walifyatua mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji pembezoni mwa mkutano mkubwa wa kupinga mpango wa kufunga mkaja. Mwanamme mmoja mwenye umri wa miaka 65 alizirai na kufa kutokana na mshtuko wa moyo lakini haikubainika haraka kama kifo hicho kilitokana na mabomu ya kutoa machozi.

Kwingineko katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, Rais wa Umoja huo, Herman Van Rompuy, aliwaalika wanachama wote 27 wa Umoja wa Ulaya kuhudhuria hafla ya mwezi Desemba ya kutuzwa tuzo ya amani ya Nobel mjini Oslo, Norway. Viongozi hao leo wanakutana kujadili uhusiano na China na kujadili pamoja na mizozo ya Syria, Mali na Iran.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri:Josephat Charo.