1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria: Tuko tayari kwa mazungumzo ya kuondoka Assad

Admin.WagnerD22 Agosti 2012

Syria imesema iko tayari kujadili juu ya kuondoka madarakani kwa Rais Bashar al Assad kama sehemu ya makubaliano ya kupunguza ongezeko la machafuko.

https://p.dw.com/p/15u6D
Syria
Syrische KurdenPicha: AP

Kauli hiyo ya ghafla na ya kushtusha imetolewa na Naibu Waziri Mkuu wa Syria, Qadri Jamil, alipoitembelea Urusi mara baada ya nchi hiyo kuyaonya mataifa ya magharibi kuhusu kuivamia Syria kufuatia onyo la Rais Barack Obama wa Marekani, kuhusu matumizi ya silaha za sumu.

Pamoja na kutoa kauli hiyo, Jamil ameonya kuwa kujiuzulu kwa Rais Assad kisiwe kigezo pekee cha kuleta amani nchini Syria. Jalil amesema na hapa ninamkunukuu, "Linapohusika suala la kujiuzulu, kulifanya pekee kuwa ndio kigezo kikubwa cha kufanyika mazungumzo ya amani, hiyo ina maana kuwa kamwe hautaweza kufikia katika mazungumzo hayo," mwisho wa kumnukuu.

Jalil ameongeza kuwa tatizo lolote linaweza kujadiliwa wakati wa mazungumzo na kwamba utawala wa Syria uko tayari hata kujadili suala la kuachia ngazi Rais Assad.

Rais wa Syria Bashar al-Assad (katikati) akifanya ibada msikitini.
Rais wa Syria Bashar al-Assad (katikati) akifanya ibada msikitini.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia nchini Syria, Jalil alipelekwa Urusi kujadili uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa rais ambao wagombea wote wataruhusiwa kuwania kiti hicho akiwemo rais Assad. Baraza la Kitaifa la Syria limesema kuwa linatathmini hatua ya kuunda serikali ya mpito nchini humo, lakini halikuweka wazi kama itajumuisha wanasiasa kutoka utawala wa sasa au la.

Marekani yasema Jalil hana jipya

Marekani imejibu kauli hiyo ya Jalil ambapo msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo, Victoria Nuland, amesema kuwa wameiona ripoti ya kiongozi huyo aliyoitoa kwa waandishi wa habari na hawaoni jambo lolote jipya na la kushtua.

Nuland amesema kuwa nchi yake inaamini kuondoka haraka madarakani kwa rais Assad kutatoa fursa kubwa ya kupiga hatua nyingine ya kurejesha hali ya amani nchini Syria.

Victoria Nuland, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani
Victoria Nuland, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya MarekaniPicha: Getty Images

Mauwaji yanaendelea nchini humo ambapo ripoti za mashirika ya kutetea haki za binaadamu zinaarifu kuwa mamia ya watu wameuawa kuanzia jana hadi hii leo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus. Vikosi vya serikali vimevishambulia kwa mizinga vitongoji vya mji huo ambapo watu 198 wameuawa.

Mashambulizi yamehamia mazikoni

Sasa vikosi hivyo vinawalenga watu kwenye maziko na kuwashambulia. Mamia ya miili ya watu waliokufa imekutwa chini ya jengo la msikiti wa Maadamiyat al Sham mjini Damascus baada ya kushambuliwa kwa mabomu hapo jana wakati wa ibada ya maziko.

Katika mji wa kaskazini wa Aleppo mashambulizi baina ya vikosi vya serikali na waasi bado yanaendelea ambapo wanawake na watoto wengi wanaripotiwa kuuwawa.

Mshambulizi mjini Damascus
Mshambulizi mjini DamascusPicha: Reuters

Shirika la misaada la Marekani, USAID, linasema kuwa kiasi ya watu milioni 2.5 wamekwama nchini humo na wanahitaji msaada wa kibinaadamu. Shirika hilo limeielezea hali ya machafuko nchini humo kuwa ni mbaya sana na haliwajawahi kushuhudia hali hiyo hapo kabla.

Mwandishi: Stumai George/DPAE/AFPE

Mhariri: Josephat Charo