Syria na Urusi zasitisha mashambulizi Aleppo
18 Oktoba 2016Waziri wa ulinzi wa Urusi amesema kwamba ndege za kivita za Syria na Urusi zimesitisha mashambulizi yao ya anga leo katika mji uliozingirwa wa Aleppo katika matayarisho ya usitishaji wa muda wa mapigano ambao Urusi ilitangaza kwamba utaanza baadaye wiki hii.
Kwa mujibu wa waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu , usitishaji wa mashambulizi ya anga utasaidia katika kusafisha njia kwa wanamgambo kuondoka katika maeneo ya mashariki yanayodhibitiwa na waasi katika mji huo.
Mashambulizi ya anga ya majeshi ya Urusi na Syria dhidi ya Aleppo yamesitishwa mapema leo asubuhi, Shoigu alisema , akielezea usitishaji huo wa muda kuwa ni matayarisho ya kufungua maeneo maalum kwa waasi kuondoka mjini Aleppo ifikapo Alhamis, ambapo Urusi ilitangaza , usitishaji mapigano kwa sababu za kiutu kati ya mbili asubuhi hadi saa kumi jioni kwa saa za Syria kuruhusu raia na wanamgambo kupata njia salama ya kupita kutoka katika mji huo.
Mwakilishi maalum wa Urusi katika Umoja wa mataifa Vitali Churkin ambaye anashikilia kwa sasa urais wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kupokezana alitangaza hatua hiyo katika Umoja wa Mataifa jana.
"Sisi tumetangaza masaa manane ya kusitisha mapigano. Nadhani kwamba usitishaji mrefu zaidi kama masaa 48 ama 72 utahitaji aina fulani ya makubaliano ya pande zote."
Katika wakati huo , majeshi ya Syria na Urusi yatajizuwia kuchukua hatua yoyote ya mashambulio. Waasi wa Syria , ikiwa ni pamoja na wanamgambo wa al-Qaeda , pamoja na waliojeruhiwa na wagonjwa wataruhusiwa kuondoka kwenda katika jimbo jirani linalodhibitiwa na waasi la Idlib.
Ushawishi wa mataifa kwa waasi
Waziri Shoigu ameongeza kwamba , Urusi inayaomba mataifa yenye ushawishi kwa waasi mashariki mwa Aleppo kuwashawishi viongozi wao kuacha mapigano na waondoke kutoka mji huo. Ameongeza kwamba majeshi ya Syria yatarejea nyuma hadi katika maeneo ambayo yataruhusu waasi kupita bila matatizo kwa wale wenye silaha kupitia maeneo mawili , ikiwa ni pamoja na barabara kuu muhimu ya Castello.Juhudi hizo za Urusi pia zitatoa nafasi bora kwa mazungumzo baina ya wataalamu wa kijeshi kutoka mataifa mbali mbali ambayo yanatarajiwa kuanza mjini Geneva kesho Jumatano.
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Stephane Dujarric alisema baada ya kutopatikana hatua ya maana katika mashauriano ya faragha yaliyofanyika katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo la Syria kwamba kilichotakiwa ni kupata uwezekano wa kupunguza matumizi ya nguvu.
"Upunguzaji wa ghasia , kupunguza mapigano, usitishaji wa aina yoyote ambao utekelezaji wake utakuwa muhimu sana. Tumekuwa tukitoa wito wa usitishaji wa masaa 48 ili kupeleka misaada ya kiutu.
Katika mkutano mwishoni mwa wiki uliosimamiwa kwa pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergey Lavrov na John Kerry wa Marekani , mawaziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia, Uturuki na Qatar walisema watafanyakazi kuwatenganisha makundi ya upinzani yenye msimamo wa wastani mjini Aleppo kutoka kundi washirika wa zamani wa al-Qaeda katika mzozo wa Syria kama al-Nusra Front.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Daniel Gakuba